Al Houthi: Saudi Arabia ijifunze kutokana na kushindwa Marekani huko Afghanistan
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i73706-al_houthi_saudi_arabia_ijifunze_kutokana_na_kushindwa_marekani_huko_afghanistan
Mjumbe wa ngazi ya juu wa Baraza la Kisiasa la harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia unapaswa kujifunza na kupata ibra kutokana na tajiriba ya kushindwa na kufeli Marekani huko Afghanistan.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 20, 2021 00:06 UTC
  • Al Houthi: Saudi Arabia ijifunze kutokana na kushindwa Marekani huko Afghanistan

Mjumbe wa ngazi ya juu wa Baraza la Kisiasa la harakati ya Ansarullah ya Yemen amesema kuwa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia unapaswa kujifunza na kupata ibra kutokana na tajiriba ya kushindwa na kufeli Marekani huko Afghanistan.

Muhammad Ali al Houthi ameandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba: Hatima ya majeshi vamizi ni kushindwa na kufeli, licha ya fedha nyingi zinazotumiwa na majeshi hayo.  

Al Houthi amesema kuwa, utawala wa Saudi Arabia unapaswa kupata ibra na funzo kutokana na matukio ya kuondoka majeshi ya Marekani huko Afghanistan na kuongeza kuwa, muungano wa utawala wa Saudia na Marekani si imara zaidi kuliko muungano wa Marekani, nchi za Ulaya na Afghanistan, na vilevile vibaraka wa utawala wa Riyadh hawana nguvu zaidi kuliko taifa la Yemen. 

Muhammad Ali al Houthi amesisitiza kuwa, Yemen inaelekea kwenye ushindi kwa azma na imani thabiti. 

Wapiganaji wa kundi la Taliban, Jumapili Agosti 15 waliingia mji mkuu wa Afghanistan, Kabul sambamba na kuanguka kwa serikali kufuatia hatua ya Rais Muhammad Ashraf Ghani kuitoroka nchi. Kuporomoka kwa serikali ya Afghanistan kunafuatia makubaliano ya amani yaliyofikiwa baina ya Marekani na Taliban mjini Doha huko Qatar Februari mwaka jana wa 2020.