Askari wa Marekani wawalaghai Waafghani wanaotaka kuondoka Kabul
Imefichuka kuwa, maafisa usalama wa Marekani walioko katika Uwanja wa Ndege wa Kabul nchini Afghanistan wanawaitisha mlungula Waafghani wanaotaka kuondoka katika mji mkuu huo.
Duru za kuaminika zimeripoti kuwa, wanajeshi hao wa Marekani wanaodhibiti Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hamid Karzai mjini Kabul tokea Agosti 15 wanawaitisha raia wa Afghanistan rushwa kati dola 500 hadi 2000, kwa yeyote anayetaka kuondoka nchini humo pasi na sababu yoyote ya msingi.
Katika sakata hilo jipya linalofichua sura isiyo ya kibinadamu ya Marekani, askari hao wa US wanafanya ufisadi huo katika hali ambayo, watu saba walifariki dunia hivi karibuni katika msongamano na mkanyagano wa kujaribu kuingia katika uwanja huo wa ndege mjini Kabul.
Haya yanajiri huku dunia ikiendelea kulaani na kusikitishwa na kitendo cha wanajeshi wa Marekani na wale wa NATO cha kutoa kipaumbele kwa shehena za silaha, mbwa na pombe badala ya kuwatanguliza mbele makumi ya maelfu ya wanawake na watoto wa Kiafghani wanaotaka kuondoka nchini humo.
Kundi la Taliban liliteka na kudhibiti Kabul Jumapili ya tarehe 15 Agosti mara tu baada ya Rais Ashraf Ghani kukimbia nchi. Weledi wa mambo wanasema, kutekwa Kabul kulikuwa na maana ya kufikia tamati uvamizi wa miaka 20 wa Marekani na nchi nyingine za Magharibi huko Afghanistan.