UN: Mazungumzo baina ya Iran na Saudi Arabia ni "muhimu sana"
(last modified Fri, 08 Oct 2021 07:29:42 GMT )
Oct 08, 2021 07:29 UTC
  • UN: Mazungumzo baina ya Iran na Saudi Arabia ni

Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, mazungumzo kati ya Iran na Saudi Arabia ni "muhimu sana".

Stéphane Dujarric ameeleza kwamba, mashauriano yanayofanyika kati ya Saudia na Iran ni muhimu sana; na kwa lugha ya uwazi kabisa ni yenye umuhimu mkubwa sana kwa amani ya eneo.

Kauli hiyo ya msemaji wa Katibu Mkuu wa UN imetolewa katika hali ambayo, siku ya Jumapili Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan alithibitisha kuendelea mazungumzo kati ya Riyadh na Tehran na akasema, ana matumaini masuala yaliyopo baina ya pande hizo mbili yatatatuliwa kupitia mazungumzo hayo.

Katika upande mwingine, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Saeed Khatibzadeh amesema, mazungumzo na Saudia yanaendelea kufanyika na yamefikia hatua nzuri sana.

Mnamo siku ya Jumatatu, maafisa wawili wa serikali ya Iraq waliliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, wawakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia wamekutana katika duru mpya ya mazungumzo mjini Baghdad.

Hivi karibuni Iraq ilitangaza kwamba, inashiriki kama msuluhishi katika mazungumzo ya kuondoa mivutano kati ya Saudia na Iran.

Duru ya kwanza ya mazungumzo kati ya Tehran na Riyadh ilifanyika takribani miezi mitano iliyopita huko Baghdad; na baada ya hapo, mji mkuu huo wa Iraq umeendelea kushuhudia duru kadhaa za mazungumzo baina ya maafisa wa nchi hizo mbili.

Mazungumzo hayo yanafanyika katika hali ambayo, Saudi Arabia inafanya kila njia ili kujinasua na kujitoa kwenye kinamasi cha vita vya miaka kadhaa ilivyoanzisha dhidi ya Yemen, vita ambavyo licha ya kupelekea makumi ya maelfu ya raia wa Yemen kuuawa na kujeruhiwa na mamilioni kuwa wakimbizi, havijaweza kufanikisha kufikiwa hata lengo moja la Riyadh na washirika wake.../

Tags