Hamas yapongeza hatua ya Malaysia kukataa kuanzisha uhusiano na Israel
(last modified Thu, 21 Oct 2021 11:36:52 GMT )
Oct 21, 2021 11:36 UTC
  • Hamas yapongeza hatua ya Malaysia kukataa kuanzisha uhusiano na Israel

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imepongeza tamko la Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia ambaye amesema nchi yake katu haitaanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Katika taarifa leo Alhamisi, Hamas imepongeza tamko la Saifuddin Abdullah, Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia ambaye amekanusha madai ya utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa eti Malaysia imeazimia kuanzisha uhusiano na utawala huo.

Hamas imemshukuru waziri huyo wa mambo ya nje wa Malaysia kutokana na msimamo wake wa kusimama pamoja na taifa la Palestina kwa ajili ya mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Siku ya Jumatano Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia alisisitiza kuwa nchi yake itaunga mkono mapambano ya kupigania ukombozi wa Palestina na itaendelea kupinga kitendo cha Israel kuendelea kukalia kwa mabavu ardhi za Palestina.

Wananchi wa Bahrain wakipinga hatua ya ufalme wa nchi yao kuanzisha uhusiano na Israel

Abdullah aidha amepinga madai ya utawala wa Kizayuni kuwa yamkini Malaysia ikatia saini mapatano ya kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni kama zilivyofanya Morocco, Bahrain, Sudan na Umoja wa Falme za Kiarabu mwaka jana.

Hivi karibuni Issawi Frej Waziri wa Ushirikiano wa Kieneo wa utawala wa Kizayuni wa Israel alidai kuwa Oman, Tunisia, Qatar na Malaysia ziko tayari kutia saini mapatano ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu.