Kufichuliwa sura mpya vya uhalifu wa Marekani nchini Syria
Gazeti la New York Times limewanukuu maafisa wa zamani wa jeshi wa Marekani, kwamba kitengo cha operesheni za siri cha jeshi la nchi hiyo kilikuwa kikiwaua mara kwa mara raia katika operesheni zilizotajwa kuwa ni dhidi ya Daesh nchini Syria.
Kitengo hicho kinachojulikana kwa jina la " Talon Anvil", kilikuwa kikifanya kazi ya kushambulia misafara, kutega mabomu kwenye magari na vituo mbalimbali kati ya 2014 na 2019. Kitengo hicho cha Talon Anvil kilikuwa kikikwepa sheria za kuwalinda raia na kuua wakulima waliokuwa wakivuna mazao yao, watoto waliokuwa wakicheza mitaani na wanakijiji waliokimbilia hifadhi katika majengo mbalimbali. Gazeti hilo la Marekani limemnukuu afisa mmoja wa Jeshi la Anga aliyefanya kazi kwenye kikosi hicho kati ya mwaka 2016 na 2018 akisema kuwa: "Wanajeshi wa Marekani wa Talon Anvil ambao hawakuwa na huruma hata kidogo walitekeleza majukumu yao kwa na ufanisi, lakini pia walifanya mashambulizi mengi mabaya."
Ripoti hiyo ya gazeti la New York Times imefichua sura mpya ya ukatili wa jeshi la Marekani nchini Syria. Kabla ya kutolewa ripoti hiyo, ilikuwa ikisemwa kuwa, mashambulizi ya anga ya Marekani yaliyokuwa yakifanyika katika fremu ya muungano wa kimataifa dhidi ya ISIS nchini Syria, yameua mamia ya raia wa nchi hiyo. Lakini sasa imebainika kwamba, vikosi vya jeshi la nchi kavu vya Marekani, hasa vikosi maalumu vya Jeshi la hilo, pia vimefanya uhalifu wa kivita dhidi ya raia wa Syria, wakiwemo watoto.

Uvamizi wa jeshi la Marekani nchini Syria umesababisha maafa mengi. Katika kisa kimoja tu, shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limesema kuwa zaidi ya raia 1,600 waliuawa kutokana na maelfu ya mashambulizi ya anga ya Marekani na washirika wake huko Raqqa kuanzia Juni hadi Oktoba 2017, lakini Washington imekataa kubeba dhima ya kuhusika na mauaji hayo. Mashambulizi mengi ya anga ya jeshi la Marekani hayakuwa sahihi na mamia ya raia waliuawa katika mashambulizi ya anga na nchi kavu. Jambo muhimu zaidi ni kwamba jeshi la Marekani kimsingi halijali maisha ya raia wakati wa operesheni za kivita, na mara zote hulitaja suala hilo kuwa ni athari ya vita. Kwa maneno mengine ni kwa, Pentagon inaamini kuwa, mauaji ya raia hayaepukiki katika vita, na kwa msingi huo hakuna karipio lolote au adhabu inayotolewa kwa askari wa Marekani wanaofanya uhalifu wa kivita, hasa mauaji ya raia wasio na hatia. Hata katika kesi nadra ambako maafisa wa jeshi la Marekani wanahukumiwa, watenda uhalifu wa kivita huachiliwa huru bila ya kuchukuliwa hatua yoyote. Suala hili halihusiani na uhalifu wa kivita uliofanyika nchini Syria pekee, bali pia linajumuisha jinai za kivita zilizofanywa na wanajeshi wa Marekani huko Iraq na Afghanistan.
Leonid Slutsky ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Kimataifa ya Duma anasema kwamba: Watu wasio na ulinzi na raia daima hutambuliwa kama "fedha za ndururu" na "hasara isiyoepukika" wakati wa operesheni za kijeshi za Marekani, na huwa wahanga wa mashambulizi ya jeshi hilo sio nchini Syria pekee lakini pia huko Iraq na Afghanistan."
Jinai na uhalifu wa Marekani nchini Syria katika muongo mmoja uliopita kimsingi vinafanyika kwa mpangilio na malengo makhsusi. Wakati wa uongozi wa Barack Obama mwaka 2011, Marekani ilianza kuyasaidia makundi ya kigaidi nchini Syria kwa lengo la kuiangusha serikali halali ya Bashar al-Assad na kudhoofisha mhimili wa muqawama na mapambano dhidi ya Wazayuni na mabeberu. Katika awamu iliyofuata, utawala wa Obama kwa kutumia kisingizio cha kupambana na kundi la kigaidi la ISIS ambalo Marekani yenyewe ndiyo mwasisi na mfadhili wake mkuu, ulianzisha operesheni za anga na nchi kavu nchini Syria mwaka 2014 na kupeleka wanajeshi wa Marekani katika ardhi ya nchi hiyo.

Hivi hivi sasa, serikali ya Biden imeendelea kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya nchi hiyo iliyoathiriwa na vita bila kuzingatia kanuni na sheria za kimataifa kama haki ya kujitawala na bila idhini ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.