Walowezi wa Kizayuni wavamia tena msikiti mtakatifu wa al-Aqswa
Makumi ya walowezi wa Kizayuni wameuvamia tena msikiti wa al-Aqswa huko Palestina na kuuvunjia heshima msikiti huo ambao ni kibla cha kwanza cha Waislamu.
Ripoti ya Palestina al-Yaum inaeleza kuwa, katika muendelezo wa hujuma na vitendo vya chuki vya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina, makumi ya walowezi wa Kiyahudi jana walivamia tena msikiti mtakatifu wa al-Aqswa.
Walowezi hao wa Kizayuni wakisaidiwa na kupewa himaya na jeshi la Israel baada ya kuingia katika eneo la ndani la msikiti huo mtakatifu walisikika wakipiga nara dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Wazayuni hao walivamia eneo hilo takatifu kupitia upande wa Babul-Magharibah na kuanza kufanya vitendo vya kichochezi.

Katika miezi ya hivi karibuni vitendo vya hujuma na uvamizii wa walowezi wa Kizayuni katika maeneo ya Wapalestina hususan katika msikiti wa al-Aqswa vimeongezeka mno.
Vitendo vya kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu huko Palestina vinafanyika katika hali ambayo, viongozi wa nchi za Kiarabu na jamii ya kimataifa wameendelea kunyamaza kimya na kutochukua hatua zozote za maana za kukabiliana na vitendo hivyo vinavyokinzana na utu na ubinadamu.
Utawala wa Kizayuni ambao unaungwa mkono kikamilifu na Marekani katika hatua zake hizo haramu umedhamiria kubadilisha muundo wa kijiografia na kidemografia wa maeneo ya Palestina; ili kwa kuyazayunisha maeneo hayo na kuhakikisha unazihodhi na kuzidhibiti kikamilifu ardhi za Wapalestina.