Israel, Misri, UAE na Jordan zapanga kumtimua Rais wa Palestina
Utawala wa Kizayuni wa Israel na waitifaki wake ikiwemo Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na Jordan zinapanga njama ya kumuondoa madarakani Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina Mahmoud Abbas.
Duru za habari zimearifu kuwa, Israel na nchi hizo za Kiarabu zinashinikiza kuondolewa madarakani Mahmoud Abbas ili nafasi yake ichukuliwe na kiongozi wa zamani wa harakati ya Fat'h, ambaye kwa sasa ni kibaraka wa nchi hizo za Kiarabu.
Tovuti ya 'Middle East Eye' imenukuu vyanzo vya habari kutokana Jordan vikisema kuwa, tayari Imarati imefanya mazungumzo na Tel Aviv kuhusu kuondolewa madarakani Abbas na wadhifa huo kuchukuliwa na Mohammed Dahlan. Tovuti hiyo imefichua kuwa, nchi tatu hizo za Kiarabu baadaye zinatazamiwa kuifahamisha Saudi Arabia kuhusu makubaliano yao na hatima ya Abbas. Katika fremu ya kufanikisha mpango huo, nchi hizo za Kiarabu pamoja na utawala haramu wa Israel zimeanza kushinikiza kuwa Dahlan ateuliwe kuwa makamu wa Mahmoud Abbas. Itakumbukwa kuwa, Dahlan ambaye kwa sasa anaishi katika Umoja wa Falme za Kiarabu alitimuliwa na harakati ya Fat'h mwaka 2011, kwa tuhuma za ufisadi wa kifedha.
Hii ni katika hali ambayo, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina ametaka kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa ambayo itafanya kazi kulingana na ratiba na mipango ya Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO).