Vikosi vya kimataifa na kuendelea kuwepo Imarati nchini Yemen
(last modified Wed, 02 Mar 2022 02:21:39 GMT )
Mar 02, 2022 02:21 UTC
  • Vikosi vya kimataifa na kuendelea kuwepo Imarati nchini Yemen

Kwa mara nyingine tena Imarati imeimarisha uwepo wake wa kijeshi usio wa moja kwa moja nchini Yemen kupitia mfumo wa vikosi vya kimataifa.

Imarati ni nchi muhimu zaidi inayopigana vita vya kichokozi dhidi ya Yemen tangu 2015 ikishirikiana kwa karibu na Saudi Arabia. Kuwepo kijeshi Imarati nchini Yemen kumeleta changamoto kubwa kwa nchi hiyo ya Ghuba ya Uajemi. Katika uwanja huo, Imarati wakati mmoja ilitangaza kwamba ilikuwa imejiondoa katika vita vya Yemen na kuondoa majeshi yake kusini mwa nchi hiyo. Januari iliyopita nchi hiyo iliamuru kuondolewa wapiganaji wake vibaraka wa  al-Amaliqa kutoka majimbo ya Ma'rib na Shabwa, na hivyo kuthibitisha kivitendo kwamba ilikuwa katika hatari kubwa ya kiusalama kutokana na ukweli kuwa Januari hiyo hiyo ilikabiliwa na mashambulio ya mara kwa mara ya Wayemen.

Hata hivyo, Imarati bado inaonekana kusisitiza kuendelea kuwepo kijeshi katika ardhi ya Yemen, lakini kupitia uwepo usio wa moja kwa moja. Kwa maneno mengine ni kuwa, Imarati inatumia mamluki kutekeleza sera zake nchini Yemen. Abu Dhabi iliwahi kutekeleza siasa hizo huko nyuma, ambapo kila ilipokabiliwa na mashambulizi kutoka kwa Wayemen, ilitekeleza siasa hizo kwa umakini mkubwa zaidi.

Majeshi ya Imarati katika ardhi ya Yemen

Kuhusiana na hilo, tovuti ya al-Khabar al-Yamani ilisema katika ripoti yake ya karibuni kwamba baada ya kukamilisha ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa ar-Rayyan ikiwa moja ya kambi muhimu zaidi za kijeshi katika Bahari  "Arabu", Imarati iliruhusu kupelekwa huko vikosi vya kimataifa. Uwanja wa ndege wa ar-Rayyan ni mojawapo ya viwanja muhimu vya ndege nchini Yemen. Tovuti hiyo imesema Imarati imepeleka mamluki wa Jordan, Sudan na Marekani katika kituo hicho cha kijeshi. Uwanja huo wa ndege ni kituo cha pili cha majeshi ya kimataifa ambacho kinatumiwa na Imarati kupeleka vifaa vya kijeshi na mamluki wake katika pwani ya mashariki ya Yemen.

Kutumiwa uwanja huo na vikosi vya kimataifa kunapunguza uwezekano wa askari wa Imarati kulengwa moja kwa moja katika vita vya Yemen, na wakati huo huo, kupunguza ushiriki wa moja kwa moja wa Imarati katika vita hivyo. Pamoja na hayo, siasa hizo haziwezi kuidhaminia Imarati usalama wake kwa sababu Serikali ya Wokovu wa Kitaifa ya Yemeni inafahamu vizuri kwamba vikosi vya kimataifa vinachukua maagizo kutoka Saudi Arabia na Imarati.

Suala jingine ni kwamba Imarati inatumia kijeshi maeneo yake inayoyakaliwa kwa mabavu dhidi ya Wayemen. Kwa hakika, ingawa maeneo hayo yanadhibitiwa na vikosi vya kimataifa vinavyoshirikiana na UAE, lakini ni wazi kuwa yanatumika kama kambi za kijeshi za Imarati. Kuhusiana na hilo, Imarati imejenga kituo cha kijeshi karibu na Uwanja wa Ndege wa ar Rayyan wa Yemen baada ya kuukalia kwa mabavu na inafuatilia malengo yake ya kijeshi kutokea hapo. Sehemu kubwa ya pwani ya al-Mukalla pia iko chini ya udhibiti wa vikosi vya kimataifa vinavyoshirikiana na Umoja wa Falme za Kiarabu UAE.

Uharibifu unaofanywa na Saudia nchini Yemen kwa ushirikiano wa Imarati

Kwa maelezo hayo, Imarati kivitendo bado haijatoka Yemen, na vikosi vya kimataifa vinavyoshirikiana nayo kwa karibu vingalipo katika maeneo ya kistratijia ya Yemen. Sababu moja ya Imarati kung'ang'ania kuendelea kuwepo Yemen inahusiana na ushindani wake na Saudi Arabia. Imarati imetumia pesa nyingi kushirikiana na Saudi Arabia katika uvamizi wake huko Yemen, na kwa hivyo haiko tayari kuondoka nchini humo bila mafanikio, na kuiona Saudi Arabia ikiendelea kuimarisha ushawishi wake katika maeneo ya kusini mwa Yemen ikiwa peke yake.