May 30, 2016 15:28 UTC
  • Bunge la Kiarabu lataka kuundwa nchi ya Palestina

Bunge la Kiarabu limeutaka Umoja wa Mataifa uhakikishe inaundwa nchi ya Palestina mji wake mkuu ukiwa ni Baitul- Muqaddas. Bunge la Kiarabu limetoa wito huo katika kikao kilichofanyika katika makao makuu ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu huko Cairo, Misri.

Ahmad Muhammad al Jarwan, Spika wa bunge la Kiarabu amesema katika ufunguzi wa kikao hicho huko Cairo kuwa, ameyataka mabunge mbalimbali duniani kususia bidhaa za utawala wa Kizayuni.

Al Jarwan pia ameuhimiza Umoja wa Mataifa na jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kutekeleza sheria za kimataifa ili kuipatia ufumbuzi kadhia ya Palestina na kuundwa nchi ya Palestina mji wake mkuu ukiwa ni Baitul Muqaddas na pia kukabiliana na siasa haramu za utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina, zinazojumuisha kuuliwa ovyo Wapalestina, kuwatia mbaroni, kuwabagua, kuzingira ardhi zao na kuendelezwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi za Palestina.

Spika wa bunge la Kiarabu pia ametaka kufikiwa makubaliano ya kusimamisha vita nchini Syria ili kuzuia kumwaga damu za raia wa nchi hiyo na kuitaka jamii ya kimataifa kutekeleza majukumu yake ya kibinadamu kuhusiana na mgogoro wa Syria.

Tags