UN: Kiwango cha njaa nchini Yemen kuongezeka mara tano mwaka huu
(last modified Tue, 15 Mar 2022 08:15:06 GMT )
Mar 15, 2022 08:15 UTC
  • UN: Kiwango cha njaa nchini Yemen kuongezeka mara tano mwaka huu

Umoja wa Mataifa unatabiri kuwa kiwango cha njaa kali nchini Yemen kitaongezeka mara tano katika mwaka huu 2022 kutokana na kuzorota kwa hali ya kibinadamu nchini Yemen.

Vita vya Saudi Arabia na waitifaki wake nchini Yemen hadi sasa vimeua na kujeruhi malaki ya Wayemen wasio na hatia na wengine milioni 4 wamelazimika kuhama makazi yao.

Kwa mujibu wa Al-Arabi Al-Jadeed, mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa, ikiwa ni pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF), Mpango wa Chakula Duniani na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), yamesema katika taarifa ya pamoja kuwa "wasiwasi sasa ni juu ya watu 31,000 nchini Yemen ambao wanakabiliwa na kiwango kikubwa cha njaa, na kiwango hicho kitaongezeka mara tano hadi 161,000 kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Siku chache zilizopita pia Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) ulitangaza kuwa, mamilioni ya watoto wa Yemen wapo katika hatari ya kupoteza maisha kutokana na kusakamwa na njaa, huku muungano wa kivita unaoongozwa na Saudi Arabia ukiendelea kufanya mashambulizi na kuliwekea mzingiro wa kila upande taifa hilo maskini la Kiarabu.

UNICEF imesema: Watoto wa Yemen wapo katika ncha ya kuaga dunia kwa njaa kali, si kutokana na uhaba wa chakula pekee, bali kutokana na familia zao kushindwa kununua chakula chenyewe masokoni.

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa, ikiwa vita vya Saudi Arabia na washirika wake havitomalizwa katika taifa hilo, basi Yemen itaelekea kwenye hali ambayo haitoweza kubadilishwa na kuingia kwenye hatari ya kupoteza kizazi kizima cha watoto nchini humo.