Kukabidhiwa Saudi Arabia faili la mauaji ya kigaidi ya Khashoggi
Huku mzozo wa kiuchumi wa serikali ya Ankara na changamoto za kifedha zikizidi kuongezeka, matatizo ya maisha ya watu wa Uturuki hatimaye yameipelekea serikali ya Recep Tayyip Erdogan kwa mara nyingine tena kushirikiana na utawala haramu wa Israel, Marekani, Misri na tawala nyingine vibaraka za Kiarabu za Ghuba ya Uajemi.
Mtazamo huo mpya wa serikali ya Erdogan unaonyesha kuwa, viongozi wa Ankara wanaamini kuwa pande hasimu ambazo zimekuwa zikihasimiana na Uturuki katika miaka michache iliyopita hususan Israel, Marekani, Misri na baadhi ya nchi za Kiarabu ndio chanzo cha mgogoro wa kiuchumi wa nchi hiyo. Kwa maelezo hayo, uamuzi wa Uturuki kuanza kushirikiana na nchi hizo unapasa kuchukuliwa kuwa ni ishara ya udhaifu na kutekelezwa sera zisizo na msingi katika uga wa kimataifa.
Kwa hakika, tunaweza kusema kwamba matamshi yote makali na mara nyingine ya kupindukia mpaka yaliyotolewa huko nyuma na rais wa Uturuki dhidi ya washirika wa Marekani katika eneo, yote hayo yalitokana na hisia za kibinafsi na huenda za kidini za Erdogan na wala hayakuwa na uhusiano wowote na sera za Uturuki za muda wa kati au mrefu.
Rais wa Uturuki alijaribu kwa mara ya kwanza kunyanyua hadhi yake katika ulimwengu wa Kiislamu wakati wa mkutano wa Davos nchini Uswisi mwaka 2008 kwa matamshi makali dhidi ya rais wa wakati huo wa utawala wa Kizayuni. Lakini pamoja na hayo msimamo huo ulisababisha mvutano na Israel na kuathiri vibaya uhusiano wa pande mbili.
Licha ya uwepo wa mivutano mingi katika uhusiano wa Uturuki na Israel, viongozi wa Ankara hawakuwahi kukata uhusiano wa kiusalama au kijeshi na Israel na wameendelea kushirikiana kwa siri na utawala huo wa kibaguzi.
Wakati huo huo, maafisa wa Uturuki hivi majuzi walijaribu kuboresha uhusiano wa pande mbili kwa kuwaachilia huru majasusi kadhaa wa Israel. Mfano wa hali hiyo umeonekana wazi katika uhusiano wa Uturuki na Misri. Hivi karibuni Uturuki ilimtuma balozi wake mpya nchini Misri baada ya kupita miaka tisa.
Sera hiyo hiyo imetekelezwa katika uhusiano wa Uturuki na Imarati au UAE. Licha ya viongozi wa Ankara, haswa Recep Tayyip Erdogan, kuituhumu UAE mara kwa mara kwamba ni moja ya nchi zilizohusika katika mapinduzi yaliyoshindwa ya Uturuki Julai 2016, hivi karibuni wamebadilisha sera zao za kigeni na kuamua kushirikiana kwa karibu na Imarati.
Wakati huo huo, juhudi za rais wa Uturuki za kuboresha uhusiano na Saudi Arabia zinaonyesha kuwa hana mfano maalumu wa uongozi anaofuata kuhusu sera za kigeni bali anaoongozwa na matamanio, maslahi ya kibinafsi na mihemko tu.
Kuhusiana na suala hilo, nafasi ya Marekani na utawala wa kibaguzi wa Israel katika kushawishi na hatimaye kuitumbukiza Uturuki katika mkondo potovu wa nchi vibaraka na tegemezi kwa Magharibi haipaswi kufumbiwa macho.
Badala ya kushirikiana na nchi huru za eneo hususan Iran na Russia, Rais wa Uturuki ameamua kushirikiana na tawala zinazopinga nchi huru za eneo yaani Marekani na Uzayuni wa kimataifa.
Hapana shaka kuwa moja ya malengo makuu ya Rais wa Uturuki katika ushirikiano huo ni kutatua mgogoro wa kiuchumi na kifedha wa serikali ya Ankara na wakati huo huo kutatua matatizo ya maisha ya watu wa nchi hiyo kabla ya kufanyika uchaguzi wa rais katika majira ya joto ya 2023.
Pamoja na hayo itakuwa vigumu kwa nchi potofu za Magharibi zikiongozwa na Marekani kutekeleza ahadi zao kwa Uturuki na kupunguza matatizo yake ya kifedha na kiuchumi. Wakati huo huo, juhudi za Uturuki kuanzisha uhusiano na Saudi Arabia zinapaswa kutathminiwa kwa mshangao.
Viongozi wa Ankara hususan Rais wa Erdogan daima wamekuwa wakidai kwamba kesi ya mauaji ya Jamal Khashoggi, mwandishi wa habari mkosoaji wa serikali ya Riyadh katika ubalozi mdogo wa Saudia mjini Istanbul itatatuliwa. Lakini hatimaye serikali ya Uturuki imeamua kuukabidhii utawala wa Riyadh nyaraka za mahakama za kesi hiyo kama sehemu ya juhudi zake za kuboresha uhusiano na Saudi Arabia.
Kuhusiana na hilo na katika hatua ya kushangaza na kushtua, mahakama ya Uturuki siku ya Alkhamisi Aprili 7 iliamua kuukabidhi utawala wa Saudia nyaraka zinazohusiana na mauaji ya kigaidi ya Khashoggi.
Katika radiamali ya kwanza kuhusu hatua hiyo, Michael Page, naibu mkurugenzi wa shirika la Human Rights Watch katika ukanda wa Mashariki ya Kati na ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya kibinadamu, amekosoa hatua hiyo ya serikali ya Ankara kwa kusema:
"Uamuzi huo wa Uturuki unahitimisha uwezekano wowote wa kutekelezwa haki na uadilifu na kuhamishiwa Saudia kesi ya mauaji ya Khashoggi kunatilia nguvu imani ya watawala wa Saudia kwamba wanaweza kukwepa mashtaka ya mauaji."
Amnesty International pia imehoji na kukosoa hatua ya hivi karibuni ya serikali ya Erdogan, kwa kusema:
"Ankara inakabidhi kesi hii kwa makusudi na kwa hiari kwa wale wanaohusika nayo (watuhumiwa wakuu)."
Kwa hitimisho la jumla, tunapasa kusema kwamba licha ya kauli mbiu na nara zote kali za viongozi wa Ankara dhidi ya serikali ya Riyadh, kesi ya mauaji ya kigaidi ya Jamal Khashoggi dhidi ya watuhumiwa 26 imefungwa rasmi nchini Uturuki na nyaraka zilizopo kuhamishiwa Saudi Arabia.
Kuhusiana na hilo, ni wazi kwamba kutokana na kuongezeka madaraka ya rais wa Uturuki, sehemu ya uhuru wa mahakama ya nchi hiyo imekabidhiwa Erdogan mwenyewe, na hatua yake ya hivi karibuni hatimaye katika muda wa kati na mrefu itakuwa na madhara kwa serikali na watu wa Uturuki. Ni wazi kuwa matatizo ya nchi hiyo na nchi za eneo yataongezeka kwa sura nyingine.