Ansarullah yakaribisha kujiuzulu Hadi, yapinga mazungumzo ya Wayemen huko Saudia
Harakati ya Ansarullah ya Yemen sambamba na kupongeza hatua ya Abdrabbuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu mwenyewe na kukimbilia Saudi Arabia kutangaza rasmi kuachia ngazi, imesema kitendo hicho kimeufanya Umoja wa Mataifa usiwe tena na kijisababu cha kuendelea kuwaunga mkono wavamizi wa nchi hiyo maskini, wakiongozwa na Saudia.
Mohammed Abdul-Salam, Msemaji wa Ansarullah amesema katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, kujiuzulu kwa Mansour Hadi kumetupilia mbali madai ya nchi zilizoishambulia Yemen kuwa zilichukua hatua hiyo kwa ajili ya kukabiliana na watu na makundi yaliyokula njama za kumpindua madarakani rais huyo mtoro.
Amesema jamii ya kimataifa na Umoja wa Mataifa hazina tena sababu ya kuendelea kutumia istilahi ya "Serikali ya Yemen Inyaotambulika Kimataifa' kwa ajili ya kuwaua kwa ummati wananchi wa Yemen na kuendelea kuwawekea mzingiro.
Msemaji wa Ansarullah amesisitiza kuwa, taifa la Yemen halitashughulishwa na mazungumzo ya makundi haramu ya eti kujadili kadhia ya nchi hiyo ya Kiarabu yanayotazamiwa kufanyika nchini Saudia.
Amesema njia pekee ya utawala wa Aal-Saud kuimarisha amani nchini Yemen ni kuachana na mashambulizi yake ya zaidi ya miaka saba, kuondoa mzingiro na kuviondoa vikosi vya muungano vamizi katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu.
Hadi alitangaza rasmi kuachia ngazi na kukabidhi madaraka kwa baraza jipya la urais katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mapema Alkhamisi, ambapo alitangaza pia kumuuzulu makamu wake, Ali Mohsen al-Ahmar.