Mazungumzo ya Iran na Saudi Arabia yaanza tena
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i82854-mazungumzo_ya_iran_na_saudi_arabia_yaanza_tena
Wawakilishi wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia wamekutana kwa duru ya tano ya mazungumzo yenye lengo la kurekebisha uhusiano uliozorota wa nchi hizi mbili jirani katika Ghuba ya Uajemi.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 23, 2022 23:20 UTC
  • Mazungumzo ya Iran na Saudi Arabia yaanza tena

Wawakilishi wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Saudi Arabia wamekutana kwa duru ya tano ya mazungumzo yenye lengo la kurekebisha uhusiano uliozorota wa nchi hizi mbili jirani katika Ghuba ya Uajemi.

Shirika la Habari la Nour News linalofungamana na Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran limeripoti kuwa, duru ya tano ya mazungumzo baina ya wawakilishi wa Iran na Saudi Arabia imefanyika hivi karibuni katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad baada ya kusitishwa mwezi Machi.

Tovuti ya Nour News imeyataja mazungumzo ya karibuni baina ya Iran na Saudia kuwa  'chanya'  na kusisitiza kuwa, pande mbili zilibadilishana mawazo kuhusu changamoto zinazozuia kurejeshwa uhusiano baina ya pande mbili.

Aidha imedokezwa kuwa mazingira chanya ya mazungumzo ya hivi karibnuni yameibua matumaini kuwa Iran na Saudia zinachukua hatua ya kurejesha tena uhusiano. Nour News pia imebaini kuwa, inatarajiwa kuwa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi mbili watakutana hivi karibuni.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian

Tovuti hiyo pia imedokeza kuwa maafisa wa ngazi za juu wa Iraq na Oman wamekuwa na nafasi muhimu katika kuandaa mikutano ya wawakilishi wa Iran na Saudia. Nchi hizi mbili kubwa za eneo la Asia Magharibi zilifanya duru nne za mazungumzo nchini Iraq kuanzia Aprili mwaka jana.

Mvutano wa Saudia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ulianza Januari 2016 baada ya Saudia kumnyonga Sheikh Nimr Baqir al-Nimr. Kufuatia kunyongwa mwanazuoni huyo, waandamanaji wa Iran waliokuwa na hasira walivamia ubalozi wa Saudi mjini Tehran. Kwa muda mrefu Saudia imekuwa ikifuata sera ya uhasama dhidi ya Iran lakini sasa inaonekana kubadili sera hiyo.