HAMAS: Wavamizi hawana nafasi kabisa katika ardhi za Palestina
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imetangaza kuwa, wavamizi hawana nafasi kabisa katika ardhi za Palestina.
Hayo yamo katika taarifa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) iliyotolewa kwa mnasaba wa mwaka wa 74 wa Siku ya Nakba ambayo inakumbushia uvamizi, mauaji ya kimbari, ukatili na jinai za Wazayuni dhidi ya Wapalestina.
Sehemu nyingine ya taarifa hiyo inaeleza kuwa, muqawama na mapambano ya silaha ndio njia pekee ya kukabiliana na jinai za kila uchao za utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina.
Kadhalika taarifa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imesisitiza kwa mara nyingine tena kuwa, njia pekee ya kuzikomboa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ni kudumishwa muqawama na mapambano.
Muqawama utaendelea hadi pale ardhi yote ya Palestina itakapokombolewa na kutobakia hata kipande kidogo cha ardhi chini ya makucha ya Wazayuni maghasibu.
Kwa upande wake pia Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina amesema kuwa, kusimama imara ndiyo njia pekee ya kukabiliana na njama za kuiyahudisha Palestina na kupambana na mauaji ya kimbari wanayofanyiwa Wapalestina.
Miaka 74 iliyopita, yaani tarehe 15 Mei 1948, magenge mbalimbali ya watenda jinai ya Kizayuni yalifanya jinai za kutisha dhidi ya wananchi wasio na ulinzi wa Palestina na kuwapora ardhi yao. Siku hiyo inajulikana kwa jina maarufu la Siku ya Nakba na nakama.