Israel yamshinikiza Biden aondea Pegasus kwenye orodha nyeusi ya US
Maafisa wa utawala wa Kizayuni wa Israel wanamshinikiza Rais Joe Biden wa Marekani afute jina la kampuni ya Israel ya NSO ambayo imekuwa ikiuza programu ya kijasusi ya Pegasus kwenye orodha nyeusi ya Washington.
Shirika la habari la Axios limenukuu maafisa wa Marekani na Israel wakisema kuwa, Washington inajiandaa kuliondoa shirika hilo la Kizayuni katika orodha yake nyeusi kufuatia mashinikizo ya Tel Aviv.
Ripoti ya shirika la Walla imenukuu afisa wa ngazi ya juu wa Israel ambaye hakutaka kutaja jina lake akisema: "Hata kama kampuni ya NSO ina matatizo na wateja wake, lakini hilo halimaanishi kuwa huduma zake hazihitajiki."
Tokea Julai mwaka jana, utawala haramu wa Israel umekuwa chini ya mashinikizo makubwa ya kimataifa ya kuutaka uache mara moja kuuza nje programu ya kijasusi ya Pegasus ya kampuni ya Kizayuni ya NSO.
Mapema mwaka huu, gazeti la New York Times liliripoti kuwa, kampuni ya Israel ya NSO imekuwa ikiuza programu ya kijasusi ya Pegasus kwa mashirika ya kijasusi na vyombo vya sheria vya nchi mbalimbali ikiwemo Marekani kwa takriban muongo mmoja ili kupeleka mbele siasa za kihasama za utawala wa Kizayuni.
Uchunguzi wa mashirika zaidi ya 17 ya habari inaonesha kuwa, programu ya kijasusi ya Pegasus, iliyotengenezwa na kampuni ya NSO ya Israel, imekuwa ikitumika kujasisi simu za mamia ya waandishi wa habari, wanaharakati wa masuala ya kisiasa na kijamii, pamoja na wanasiasa duniani kote.