Hizbullah yatoa msimamo kwa hatua ya Saudia kuifungulia Israel anga yake
Hizbullah ya Lebanon imesema, hatua ya Saudi Arabia ya kuufungulia utawala haramu wa Kizayuni wa Israel mipaka ya anga yake ni sawa na kuwa mshirika wa jinai zinazofanywa na utawala huo na ni usaliti kwa umma wa Kiislamu.
Siku ya Alkhamisi iliyopita, utawala wa Kizayuni ulipitisha vipengele viwili vya makubaliano yanayohusiana na visiwa viwili vya kistratejia vilivyoko katika Bahari Nyekundu, hatua inayotafsiriwa kuwa ni kichocheo cha kuirubuni Saudi Arabia ili ifungue njia kwa ajili ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na Tel Aviv.
Kufuatia hatua hiyo iliyochukuliwa na Israel, Saudia kwa upande wake imefungua anga yake kwa ajili ya "vyombo vyote vya usafiri wa anga".
Kuhusiana na suala hilo, mjumbe wa Baraza Kuu la Hizbullah ya Lebanon Sheikh Nabil Qaouq amesema, wakati Saudi Arabia inapoziruhusu ndege za Isreal zipite juu ya anga ya Haram Mbili tukufu za Makka na Madina huwa inawatusi na kutonesha hisia zao Waisamu bilioni moja na milioni mia nane duniani.
Sheikh Qaouq ameongeza kuwa, wakati Saudia inaposhirikiana kiusalama na kijeshi na utawala wa Kizayuni inakuwa mshirika wa uchokozi unaofanywa na utawala huo dhidi ya Syria, Lebanon na Palestina; na hilo pekee linatosha kuwa usaliti kwa wananchi wa mataifa hayo ya Waislamu.
Sambamba na hatua hiyo iliyochukuliwa na Saudi Arabia, waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Faisal bin Farhan amedai kuwa kuondolewa kizuizi yalichokuwa yameekewa mashirika ya ndege ya utawala wa Israel ya kupitisha ndege zao katika anga ya Saudia hakuna mfungamano wowote na suala la uhusiano wa Riyadh na utawala wa Kizayuni.../