Saudia yaahidi kuipatia Ukraine msaada wa dola milioni 400
Oct 15, 2022 22:54 UTC
Saudi Arabia imeahidi kuipatia Ukraine msaada wa dola milioni 400 kwa ajili ya masuala ya kibinadamu.
Kwa mujibu wa Reuters, shirika rasmi la habari la Saudi Arabia limetangaza kuwa nchi hiyo itaipatia Ukraine msaada wa dola milioni 400 kwa ajili ya masuala ya kibinadamu.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mrithi wa ufalme wa Saudia Mohammed bin Salman amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na kumweleza katika mazungumzo yao hayo kuwa Riyadh itaipatia Kiev msaada wa dola milioni 400 fedha taslimu.
Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine naye pia ametangaza kuwa amefanya mazungumzo kwa njia ya simu na Mohammed bin Salman na kubainisha kwamba, amefikia makubaliano na mrithi wa ufalme wa Saudia kushirikiana katika suala la kuachiliwa huru mateka wa vita na vilevile kuipatia nchi yake msaada wa fedha.
Kabla ya hapo, Saudi Arabia ilihusika katika usuluhishi wa kusimamia mchakato wa kubadilishana mateka wa vita kati ya Russia na Ukraine.
Hadi kufikia sasa, nchi nyingi zimetangaza utayari wao wa kupatanisha kati ya Ukraine na Russia ili kumaliza vita vinavyoendelea baina ya nchi hizo mbili, lakini juhudi hizo hadi sasa bado hazijazaa matunda.../
Tags