Qatar yataka kuhitimishwa ukaliaji mabavu wa utawala wa Kizayuni
Mwakilishi wa Kudumu wa Qatar katika Umoja wa Mataifa leo asubuhi amehutubia katika kikao cha kiduru cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusema: Israel inapasa kuhitimisha hatua zake za kuzikalia kwa mabavu ardhi za Waarabu ikiwemo miinuko ya Golan huko Syria, ardhi za Lebanon na Palestina.
Bi Alia Al Thani Mwakilishi wa Kudumu wa Qatar katika Umoja wa Mataifa amesema: ufumbuzi wa kuasisi nchi mbili huru ni njia bora ya kutatua kadhia ya Palestina. Alia Al Thani amesisitiza pia udharura wa kusitishwa haraka ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni, kurejea wakimbizi wa Kipalestina, kulinda haki za kihistoria za watu wa Palestina na kuunda taifa huru la Palestina.
Amesema: njia bora ya kufanikisha lengo hilo ni kufanyika mazungumzo kati ya pande mbili na kwamba jamii ya kimataifa inapasa pia kuchukua hatua za kuharakisha mchakato wa amani na kutatua masuala yote yanayoibua mzozo.
Mwanadiplomasia huyo wa Qatar amesema, mji wa Quds ni kati ya kadhia muhimu sana kwa ajili ya kufikia ufumbuzi wa mwisho. Ametahadharisha pia juu ya uvurugaji wowote wa hali ya kihistoria na kisheria wa maeneo matakatifu ya Kiislamu na Kikristo katika mji huo.
Mwakilishi wa Kudumu wa Qatar katika Umoja wa Mataifa ameeleza haya huku katika siku za karibuni wanajeshi wa utawala wa Kizayuni wakiwa wamevamia pakubwa miji kadhaa ya Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuwaua shahidi, kuwajeruhi na kuwatia nguvuni Wapalestina kadhaa.