Sheikh Isa Qassim: Uchaguzi ujao unalenga kuimarisha udikteta Bahrain
(last modified Fri, 04 Nov 2022 02:24:02 GMT )
Nov 04, 2022 02:24 UTC
  • Sheikh Isa Qassim: Uchaguzi ujao unalenga kuimarisha udikteta Bahrain

Kiongozi mashuhuri wa kidini nchini Bahrain amesema uchaguzi ujao wa Bunge nchini humo hauna lengo jingine isipokuwa kuimarisha mienendo ya kiimla na kidikteta ya watawala wa Aal-Khalifa.

Sheikh Isa Qassim, kiongozi wa kidini wa mapinduzi ya Bahrain amesema hayo katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter hapo jana na kuongeza kuwa: Chaguzi nchini Bahrain zinakusudia kuimarisha udikteta, lakini watu wanatumbukia kwenye mchezo huo wa ukoo unaotawala.

Ayatullah Sheikh Isa Qassim amesisitiza juu ya upinzani wa wananchi wa Bahrain dhidi ya uchaguzi wa Bunge wa nchi hiyo na kufafanua kwamba, mchakato wa uchaguzi ujao wa nchi hiyo ni wa kidhulma na sio wa kiadilifu. Amehoji kwa kusema, "Je, mantiki inahukumu kushiriki katika chaguzi za namna hii?" 

Kabla ya hapo, mrengo mkubwa zaidi wa upinzani nchini humo ulitangaza kususia uchaguzi huo. Chama cha Kiislamu cha al-Wefaq kimetoa mwito kwa Wabahrain kususia uchaguzi wa Bunge nchini Bahrain ambao umepangwa kufanyika Novemba 12. 

Bahrain imeshuhudia harakati za mapinduzi ya wananchi tokea Februari 14 mwaka 2011 dhidi ya utawala wa Al Khalifa. Wabahrain wanataka kuwa huru, wanataka serikali itende uadilifu, kukomesha ubaguzi wa kimatabaka, na kuruhusu kuingia madarakani serikali itakayochaguliwa na wananchi. 

Wabahrain katika maandamano ya kupinga ukoo wa Aal-Khalifa

Makundi ya kutetea haki za binadamu yametoa taarifa mara kadhaa kulaani ukandamizaji unaofanywa na utawala wa Bahrain dhidi ya wapinzani na kutoa mwito wa kufanyika mageuzi katika mfumo wa kisiasa wa nchi hiyo.

Kwa mujibu wa al-Wefaq, kukosekana serikali ya kweli nchini Bahrain kumeufanya utawala wa Aal-Khalifa uendelee kuwatwisha Wabahrain malengo yao ya kisiasa, kiuchumi, kiusalama na kijamii.