Abbas Araghchi: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono Cuba dhidi ya vikwazo vya Marekani
(last modified Sun, 22 Sep 2024 07:20:49 GMT )
Sep 22, 2024 07:20 UTC
  • Abbas Araghchi: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono Cuba dhidi ya vikwazo vya Marekani

Abbas Araghchi, Waziri Mambo ya Nje wa Iran amesema, Jamhuri ya Kiislamu ikiwa mmoja wa wahanga wakuu wa vikwazo vya Marekani, inaelewa kikamilifu hali ya watu wa Cuba, hivyo inaiunga mkono nchi hiyo dhidi ya vikwazo vya nchi hiyo ya Magharibi.

Sayyid Abbas Araghchi amekutana na Bruno Rodríguez Parrilla, Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba pambizoni mwa kikao cha 79 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, ambapo amelaani hatua ya upande mmoja na ya kisiasa ya Kongresi ya Marekani ya kuiweka Cuba katika orodha ya nchi zinazodaiwa kufadhili ugaidi na kusema hatua hiyo ni muendelezo wa hatua za kisiasa za Marekani dhidi ya nchi hiyo.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kushirikiana na Cuba ili kupanua uhusiano wa pande mbili katika nyuga mbalimbali.

Akielezea hali ya sasa katika eneo la Asia Magharibi, Araghchi aidha amefafanua kuwa jinai za utawala wa Kizayuni huko Ukanda wa Gaza na Lebanon zinatokana na kukata tamaa na kushindwa utawala huo katika medani ya vita huko Gaza.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran: Tunaunga mkono Cuba dhidi ya vikwazo vya Marekani

Kwa upande wake Bruno Rodríguez Parilla, Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba amekaribisha kuendelezwa uhusiano wa pande mbili katika nyanja za kiuchumi, kielimu na kisayansi kati ya Tehran na Havana na vilevile kuandaliwa vikao vya kamisheni ya pamoja ya kiuchumi kati ya pande mbili  na kusema Cuba inaiunga mkono Jamhuri ya Kiislamu ya Iran dhidi ya siasa za uhasama za Marekani.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia amekutana na kuzungumza na Abdullah Ali Elahia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kuwait,  ambapo amesema kuwa utawala ghasibu wa Israel ni hatari kubwa kwa amani na usalama wa eneo na dunia nzima na kuwa nchi za eneo lazima zishirikiane kwa ajili ya kuzuia ukatili wa utawala huo.

Abbas Araghchi  amesisitiza kuwa siasa za ujirani mwema ni moja ya misingi mikuu ya serikali ya awamu ya 14 ya Iran na kuwa uhusiano wa Iran na nchi za eneo utazidi kuimarika katika serikali hii mpya.

Katika muendelezo wa mikutano yake ya pande mbili mjini New York, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran pia amekutana na kuzungumza na Abdul Latif bin Rashid Al Zayani Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Bahrain na kuzungumzia masuala na mahusiano ya pande mbili, ya kieneo na kimataifa.

Tags