Iran: Kupanuka jinai za Wazayuni ni tishio kwa amani na usalama wa dunia
(last modified Mon, 29 Jul 2024 12:53:50 GMT )
Jul 29, 2024 12:53 UTC
  • Iran: Kupanuka jinai za Wazayuni ni tishio kwa amani na usalama wa dunia

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa kupanuka na kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza ni tishio kwa amani na usalama wa eneo la Maghahribi mwa Asia na dunia.

Ali Bagheri Kani, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameshiria hali ya sasa ya Gaza na jinai zinazoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya wananchi wa Palestina na kusema kuwa, jambo hilo ni kadhia muhimu zaidi ya kibinadamu duniani. Amesema, kuendelea, kushtadi na kupanuka jinai za Wazayuni dhidi ya Gaza ni mfano wa wazi wa jinai za kivita na dhidi ya binadamu;  na wote tunapasa kuzidisha jitihada ili kuzuia jinai hizo.

Ali Bagheri Kani ameeleza haya leo Jumatatu mjini Tehran katika mazungumzo yake na Elio Rodriguez Perdomo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba. 

Bagheri Kani amesema Cuba ina msimamo na mtazamo chanya kwa matukio ya Palestina na amesisitiza kuendelezwa mashauriano ili kukomesha jinai na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni. 

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Ali Bagheri Kani 

Katika mazungumzo hayo, Elio Rodriguez Perdomo Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba amesema kuwa Waziri Mkuu wa Cuba atashiriki katika hafla ya kuapishwa Rais mpya wa Iran na kwamba hiyo inaonyesha azma na jitihada za  Cuba kwa ajili ya kustawisha uhusiano kati ya Havana na Tehran. 

Perdomo pia amesema kuwa Cuba iko tayari kikamilifu kushirikiana na serikali na viongozi wapya wa Iran ili kuimarisha uhusiano wa pande wa pande mbili na pande kadhaa. 

Tags