Araqchi aionya Israel: Iran ina mbinu za kulinda taasisi zake za nyuklia
(last modified Tue, 22 Oct 2024 15:23:38 GMT )
Oct 22, 2024 15:23 UTC
  • Araqchi aionya Israel: Iran ina mbinu za kulinda taasisi zake za nyuklia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameuonya utawala wa Kizayuni Israel dhidi ya kufanya mahesabu mabaya na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inategemea zana za kijeshi zilizotengenezwa hapa nchini na pia mbinu mbalimbali ili kulinda taasisi zake za nyuklia zenye malengo ya kiraia.

Sayyid Abbas Araqchi amesema haya leo katika mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Kuwait. 

"Hakuna jinai na uhalifu ambao Israel haijaufanya hadi sasa. Kwa bahati mbaya utawala huo unaendelea kutekeleza jinai hizo ikiungwa mkono na Marekani na nchi za Ulaya", amesema Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran. 

"Baadhi ya ukatili huu unatambuliwa kama uhalifu wa kivita na unaweza kufuatiliwa katika Mahakama ya Kimataifa", amesema mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Vikosi vya ulinzi vya Iran vinafuatilia kwa karibu na kila mara mienendo yote ya wanajeshi wa Marekani ardhini na angani katika eneo zima la Magharibi mwa Asia; adui Mzayuni anajua jibu atakalopata iwapo miundombinu yetu muhimu itashambuliwa."

"Marafiki zetu wametupa hakikisho kwamba hawataruhusu ardhi  wala anga zao kutumika kufanya mashambulizi dhidi ya Iran. Nchi zote za kikanda zimesema kuwa zinapinga shambulio lolote dhidi ya Iran na taasisi za nyuklia za nchi hii", amesema Araqchi.

Tags