Kuunga mkono Iran maamuzi ya wananchi na muqawama wa Palestina
(last modified Wed, 04 Sep 2024 12:41:12 GMT )
Sep 04, 2024 12:41 UTC
  • Kuunga mkono Iran maamuzi ya wananchi na muqawama wa Palestina

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ametangaza kuwa, Tehran inaunga mkono makubaliano na uamuzi wowote wa makundi ya muqawama na wananchi wa Palestina.

Sayyid Abbas Araghchi amesema hayo katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ireland, Micheál Martin ambapo akiashiria uungaji mkono wa Iran kwa juhudi zinazoendelea za kusimamisha vita huko Gaza, amesema kuwa, Tehran inaunga mkono makubaliano yoyote ya makundi ya muqawama na wananchi wa Palestina.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran pia amesema kuwa, Tehran itaunga mkono makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano yatakayokubaliwa na Wapalestina na Harakati ya Muqawama  wa Kiiislamu wa  Palestina (HAMAS).

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema pia kuwa, jamii ya kimataifa lazima ichukue hatua za "haraka na madhubuti" za kukomesha jinai na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni huko Gaza.

Araghchi ameongeza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kuondolewa hali ya wasiwasi katika eneo hili, lakini utawala wa Kizayuni unalenga kueneza ghasia na kuzieneza katika maeneo mengine ukiwemo Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan. Kwa upande wake Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Ireland akielezea wasiwasi wake juu ya kuenea kwa hali ya wasiwasi katika eneo la Asia Magharibi amesema kuwa, nchi yake inataka kusitishwa mara moja kwa vita huko Gaza na kubadilishana mateka sambamba na kufikishwa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Gaza haraka iwezekanavyo.

Zaidi ya watu 40,000 wa Gaza wameuawa shahidi na takriban laki moja kujeruhiwa katika mashambulizi ya Wazayuni huko Gaza ambapo asilimia 70 kati yao ni wanawake na watoto. Kulingana na ripoti za kimataifa, mauaji ya Wapalestina huko Gaza ni aina mbaya zaidi ya mauaji ya kimbari na ya watoto wachanga kuwahi kufanywa katika historia ya mwanadamu.

Nembo za makundi ya muqawama wa Kiislamu

 

Ni kwa ajili hiyo ndio maana tangu kuanza duru mpya ya hujuma ya kijeshi tarehe 7 Oktoba mwaka jana (2023) na duru mpya ya mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza, mara kadhaa maafisa wakuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wameeleza wasiwasi wao kuhusu kuendelea jinai hizo dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina, na kusisitiza haja ya kukomesha jinai za utawala huo ghasibu. Juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, baadhi ya nchi na jumuiya za kimataifa za kusimamishwa jinai za utawala wa Kizayuni wa Gaza zinafanyika huku Wazayuni wakiendelea na jinai zao kwa uungaji mkono wa Marekani.

Juhudi za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na jumuiya ya kimataifa za kusimamisha jinai za utawala wa Kizayuni wa Gaza na eneo hili zinafanyika katika hali ambayo, katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita utawala bandia wa Israel umekuwa ukikwamisha mazungumzo ya usitishaji vita kwa visingizio mbalimbali sambamba na kushadidisha mashambulizi dhidi ya Gaza ili kwa njia hiiyo uweze kufikia malengo yake ya kisiasa na kijeshi katika ardhi ya Palestina.

Wakati huo huo waungaji mkono wa nchi za Magharibi wa utawala wa Kizayuni hususan dola la kibeberu la Marekani wamekuwa wakidai mara kwa mara kuunga mkono mazungumzo ya usitishaji vita huko Gaza na kwa upande mwingine bado wanaendelea kuupa utawala huo silaha haribifu kwa lengo la kushadidisha mauaji ya kimbari ya Wapalestina katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa maoni uliofanywa na Kanali 12 ya Televisheni ya utawala wa Kizayuni, asilimia 54 ya Wazayuni wanaamini kuwa, sababu ya kutomalizika vita vya Gaza ni malengo ya kisiasa ya Waziri Mkuu wa utawala huo Benjamin Netanyahu. Ukweli wa mambo ni kuwa, kwa kurefusha vita Netanyahu anajaribu kutimiza ahadi zake mwanzoni mwa vita hivyo ikiwa ni pamoja na kuiangamiza kikamilifu Hamas na kambi ya muqawama na kudhibiti usalama wa eneo hili.

 

Kuendelea ukwamishhaji mambo wa Wazayuni katika mazungumzo ya kusitisha mapigano kumeifanya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina "Hamas" kutilia mkazo utekelezwaji wa matakwa halali ya wananchi wa Palestina. Kuondoka wavamizi hao kutoka Gaza na kurejea wakimbizi wa Kipalestina ni miongoni mwa masharti makuu ya Wapalestina katika mchakato wa mazungumzo hayo. Kwa kutilia maanani matukio katika medani ya vita vya Gaza, inapaswa kuashiria ukweli huu kwamba, makundi ya wanamapambano wa Palestina yataendelea na muqawama na mapambano yao hadi matakwa yao halali yatakapotimizwa, na bila shaka hadaa na uongo wa utawala wa Kizayuni na muungaji mkono wake serikali ya Marekani hautakuwa na taathira katika mchakato wa mazungumzo ya kusitisha mapigano.

Katika mazingira kama haya, hapana shaka kwamba, kusaidia kuimarisha amani na uthabiti wa eneo ni moja ya vipengele muhimu vya siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na imeelekeza nguvu na juhudi zake zote ili kulifanikisha hilo. 

Zaidi ya Wapalestina 40,000 wameuawa shahidi tangu kuanza hujuma na mashambulio ya kinyama ya utawala haramu wa Israel katika Ukanda wa Gaza Oktoba 2023.

 

Hata hivyo, miongoni mwa mambo yanayozua mvutano na kuleta mgogoro ni utawala wa Kizayuni wa kibaguzi, unaoendelea na mauaji ya watu wa Gaza na mauaji ya viongozi wa muqawama ndani na nje ya ardhi za Palestina. Hatua hizo za Israel ni muendelezo wa mauaji ya kimbari dhiodi ya Wapalestina. Hadi sasa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limekuwa likifuatilia juhudi kubwa za kuhitimisha jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza ambazo hazijazaa matunda hadi sasa kutokana na uungaji mkono wa Marekani kwa utawala wa Kizayuni.

Kwa hakika uungaji mkono wa Wamagharibi kwa jinai za Wazayuni unaonyesha misimamo kindumakuwili ya Wamagharibi katika kadhia ya Palestina na vita vya Gaza vinaonyesha unafiki wao katika uga wa haki za binadamu katika wakati huu muhimu. Licha ya mashinikizo na matatizo yote, kipindi hiki kigumu bila shaka kitapita kwa Wapalestina na eneo hili, lakini namna na utendaji pamoja na utekelezaji majukumu wa nchi moja moja na mashirika ya kimataifa kuhusiana na mauaji hayo ya kimbari ni mambo ambayo yatarekodiwa na kubakia katika kumbukumbu za historia.