Mamia ya nyumba za Wapalestina zimebomolewa tangu kuanza mwaka huu (2022)
Mamia ya nyumba za wananchi wa Palestina zimebomolewa na utawala haramu wa Israel tangu kuanza mwaka huu wa 2022 katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds inayokaliwa kwa mabavu.
Amir Dawood, afisa wa Kamati ya Muqawama ya kukabiliana na ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni amesema kuwa, mwaka huu unaomalizika wa 2022 ulikuwa mgumu mno kwa Wapalestina kwani Israel imebomoa nyumba 850 za Wapalestina.
Aidha amesema, mbali na nyumba na makazi ya Wapalestina kubomolewa, utawala ghasibu wa Israel umebomoa pia majengo ya biashara na viwanda sambamba na kuharibu mashamba ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na kuzifanya mamia ya familia za Kiplestina kubakia bila makazi na hivyo kuishi kwa kutangatanga.
Vitendo vya kubomoa nyumba za Wapalestina vinavyofanywa na utawala ghasibu wa Israel vimekuwa vikishuhudiwa kila mwaka huko Palestina huku asasi za kimataifa zikiwa watazamaji tu wa unyama huo.
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, mwaka juzi 2020 utawala wa Kizayuni wa Israel ulibomoa nyumba karibu 689 katika Ukingo wa Magharibi na Quds tukufu na kuzilazimisha mamia ya familia za Wapalestina kuwa wakimbizi.
Hayo yanaripotiwa katika hali ambayo, hadi sasa utawala wa Israel haujachukua hatua yoyote ya kutekeleza azimio nambari 2234 la tarehe 23 Disemba 2016 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kusitishwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.
Mwezi Julai mwaka huu, Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine tena ulipitisha azimio linalosisitiza kuwa utawala haramu wa Kizayuni wa Israel hauna haki ya kupora rasilimali za watu wa Palestina na za miinuko ya Golan ya Syria unayoikalia kwa mabavu.