Mar 03, 2023 07:45 UTC
  • UNICEF: Watoto milioni 3.7 walioathirika na zilzala Syria wana hali mbaya

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF amesema, watoto milioni 3.7 ambao walinusurika na matetemeko ya ardhi ya tarehe 6 Februari mwaka huu katika maeneo yaliyoathirika nchini Syria wanakabiliwa na ongezeko la vitisho kadhaa vya zahma kubwa.

Bi Catherine Russell ameyasema hayo baada ya kukamilisha ziara yake ya siku mbili nchini humo.

Ameongeza kuwa athari za kihisia na kisaikolojia za matetemeko hayo kwa watoto ni tishio kubwa la magonjwa ya kuambukiza na yanayotokana na  maji kwa familia zilizolazimika kuhama makwao, na ukosefu wa huduma za msingi kwa familia zilizoachwa hatarini kwa sababu ya takriban miaka 12 ya vita vinaleta hatari inayoendelea na kuzidisha majanga kwa watoto walioathirika. 

Bi Catherine Russell akiwa na watoto walioathirika na zilzala wakati wa ziara yake nchini Syria

"Watoto wa Syria tayari wamevumilia mshtuko usioelezeka na madhila makubwa. Sasa, matetemeko haya ya ardhi hayakuharibu tu nyumba, shule na mahali kwa watoto kucheza, pia yamebadili kabisa hali ya usalama kwa watoto wengi na familia zilizo hatarini zaidi, " amebainisha Bi Russel.

Mkurugenzi huyo wa UNICEF amesisitiza kwa kusema: "haitoshi tu kutoa ahueni ya haraka kwa waathirika, lazima tujitolee kusimama na familia hizi kwa muda mrefu, kuzisaidia kurejesha hali ya utulivu na matumaini. Kwa ufikishaji wa huduma muhimu, kama maji salama, huduma za afya, na usaidizi wa kisaikolojia, tunaweza kusaidia watoto na familia kujikwamua kutoka kwenye jinamizi ambalo wamelivumilia ili waanze kujenga upya maisha yao." 

Nchini Syria, UNICEF inahitaji dola milioni 172.7 ili kutoa msaada wa haraka wa kuokoa maisha kwa watu milioni 5.4, wakiwemo watoto milioni 2.6, walioathiriwa na tetemeko la ardhi.../

Tags