Ufunguzi wa ubalozi wa Saudia mjini Damascus baada ya miaka 12
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i95316-ufunguzi_wa_ubalozi_wa_saudia_mjini_damascus_baada_ya_miaka_12
Vyanzo vya kuaminika vinasema kwamba Saudi Arabia inapanga kufungua tena ubalozi wake mjini Damascus baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 20, 2023 06:50 UTC
  • Ufunguzi wa ubalozi wa Saudia mjini Damascus baada ya miaka 12

Vyanzo vya kuaminika vinasema kwamba Saudi Arabia inapanga kufungua tena ubalozi wake mjini Damascus baada ya mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Saudi Arabia ilikata uhusiano wake na Syria tangu 2011 baada ya machafuko na mapigano ya ndani kuibuka nchini humo.

Vyanzo hivyo vya kuaminika vinasema kuwa upatanishi wa Russia na Imarati hatimaye umezaa matunda ambapo sasa Saudi Arabia inatazamiwa kufungua tena ubalozi wake katika mji mkuu wa Syria, Damascus, baada ya kupita miaka 12.

Duru hizo zimeongeza kuwa, baada ya makubaliano ya hivi karibuni kati ya Iran na Saudi Arabia, juhudi za nyuma ya pazia za Russia na Imarati hatimaye zimezaa matunda na kupelekea kukaribiana Saudi Arabia na Syria.

Kwa mujibu wa duru hizo za kuaminika, baada ya Eid al-Fitr, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudia Faisal Bin Farhan anapanga kuzuru Damascus na katika safari yake hiyo, atatangaza rasmi kufunguliwa tena ubalozi wa Saudi huko Damascus.

Faisal bin Farhan

Hii ni pamoja na kuwa Faisal bin Farhan alisisitiza katika kauli yake takriban siku 10 zilizopita kwamba nchi za Kiarabu zimefikia makubaliano kwamba hakuna tena haja ya kutengwa Syria, na kwamba ni lazima kufanyike mazungumzo na nchi hiyo ili kutatua matatizo yake hususan masuala ya kibinadamu.

Bin Farhan amesema kuwa zazungumzo hayo yanaweza hatimaye kupelekea Syria kurejea katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu au kwa jina jingine Arab League.

Mwaka 2011, Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ilisimamisha uanachama wa Syria katika kumuiya hiyo kutokana na mashinikizo ya Imarati na Saudi Arabia, kufuatia mapigano ya ndani nchini humo, ambapo nchi nyingine za Kiarabu pia zilifunga balozi zao na kukata uhusiano wa kidiplomasia na Damascus.