Vikosi vamizi vya US vyashambuliwa kwa maroketi mashariki ya Syria
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i95488-vikosi_vamizi_vya_us_vyashambuliwa_kwa_maroketi_mashariki_ya_syria
Kambi mbili haramu za wanajeshi vamizi wa Marekani zimeshambuliwa kwa makumi ya maroketi huko mashariki mwa Syria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 25, 2023 03:38 UTC
  • Vikosi vamizi vya US vyashambuliwa kwa maroketi mashariki ya Syria

Kambi mbili haramu za wanajeshi vamizi wa Marekani zimeshambuliwa kwa makumi ya maroketi huko mashariki mwa Syria.

Kanali ya televisheni ya al-Alam imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, vituo viwili vya askari vamizi wa Marekani vimeshambuliwa kwa maroketi 20 karibu na eneo lenye utajiri wa mafuta la al-Omar na katika medani ya gesi ya Koniko katika mkoa wa Dayr al-Zawr, mashariki mwa Syria.

Afisa wa kijeshi wa Marekani amenukuliwa na televisheni ya al-Jazeera akithibitisha habari ya kushambuliwa kambi zao hizo mashariki mwa Syria, ambapo wanajeshi kadhaa wamejeruhiwa.

Afisa huyo wa Marekani amesema Washington inatathmini hasara ya mashambulizi hayo ya maroketi dhidi ya kambi hizo. Wimbi hilo la mashambulizi ya maroketi limejiri baada ya wanajeshi hao vamizi kutekeleza hujuma dhidi ya maeneo ya raia katika mkoa huo wa mashariki.

Raia wengi wameuawa katika mashambulio ya ndege za kivita za Marekani katika mkoa wa Dayr al-Zawr mashariki mwa Syria, tangu Marekani na waitifaki wake waivamie nchi hiyo ya Kiarabu mwaka 2014.

Hujuma za US dhidi ya makazi ya raia nchini Syria

Mbali na kufanya mauaji, lakini Marekani ikishirikiana na mamluki wa Kikurdi inaendelea kuiba mafuta na rasilimali nyingine za Syria, wakati huu ambapo nchi hiyo ya Kiarabu inajaribu kujinasua kutoka kwenye misukosuko na changamoto zinazotokana na matetemeko ya ardhi yaliyoua maelfu ya watu nchini humo.

Hali kadhalika Marekani na waitifaki wake wamekuwa wakikwamisha shughuli za kufikisha misaada ya dharura na kibinadamu kwa waathirika wa zilzala nchini Syria.