Kata'ib Hizbullah: Ikilazimu, tutakabiliana moja kwa moja na Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i95556-kata'ib_hizbullah_ikilazimu_tutakabiliana_moja_kwa_moja_na_marekani
Harakati ya kupambana na ugaidi ya Kata'ib Hizbullah ya Iraq imeonya kuwa, iwapo makundi ya muqawama katika nchi hiyo ya Kiarabu yatashambuliwa na vikosi vya Marekani kama vilivyofanya Syria, basi harakati hiyo haitakuwa na budi kuingia katika makabiliano ya moja kwa moja na vikosi hivyo vamizi.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Mar 27, 2023 02:11 UTC
  • Kata'ib Hizbullah: Ikilazimu, tutakabiliana moja kwa moja na Marekani

Harakati ya kupambana na ugaidi ya Kata'ib Hizbullah ya Iraq imeonya kuwa, iwapo makundi ya muqawama katika nchi hiyo ya Kiarabu yatashambuliwa na vikosi vya Marekani kama vilivyofanya Syria, basi harakati hiyo haitakuwa na budi kuingia katika makabiliano ya moja kwa moja na vikosi hivyo vamizi.

Abu Ali al-Askari, afisa usalama wa Kata'ib Hizbullah alisema hayo jana Jumapili katika taarifa na kuongeza kuwa, vikosi vya Marekani vitakabiliwa na mashambulio ya kushtukiza iwapo vitatekeleza hujuma za anga dhidi ya maeneo ya muqawama nchini Iraq.

Amesisitiza kuwa, "Kwa mara nyingine tena tunasisitiza kuwa, Kata'ib Hizbullah itaingia katika makabiliano ya moja kwa moja na kulenga kambi za kijeshi za Marekani katika eneo zima (la Asia Magharibi), iwapo wanajeshi wa US wataamua kushambulia kambi za wanamuqawama nchini Iraq."

Alkhamisi usiku, jeshi la Marekani lilifanya mashambulizi ya anga nchini Syria, kwa madai kuwa mkandarasi wake ameuawa mbali na askari wake watano kujeruhiwa eti katika hujuma ya ndege isiyo na rubani inayodaiwa kutekelezwa na makundi ya muqawama.

Wanajihadi wa Kata'ib Hizbullah ya Iraq

Makundi ya muqawama yametekeleza mashambulizi kadhaa ya kulipiza kisasi baada ya chokochoko hizo mpya za Marekani mashariki mwa Syria. Kundi la Iraq linalojulikana kwa jina la Brigedi ya al Ghaliboun limetangaza kuhusika na shambulio dhidi ya kambi ya wanajeshi vamizi wa Marekani iliyoko mashariki mwa Syria na kutoa onyo kwa wanajeshi hao.

Raia wengi wameuawa katika mashambulio ya ndege za kivita za Marekani katika mkoa wa Dayr al-Zawr mashariki mwa Syria, tangu Marekani na waitifaki wake waivamie nchi hiyo ya Kiarabu mwaka 2014.