Waandamanaji Israel waapa, maandamano yataendelea hadi ‘mageuzi ya mahakama’ yatakapofutiliwa mbali
Kiongozi wa waandamanaji dhidi ya serikali ya utawala haramu wa Israel ameapa kuwa maandamano yataendelea katika maeneo yote yanayokaliwa kwa mabavu licha ya waziri mkuu wa utawala huo, Benjamin Netanyahu, kutangaza kuwa mpango tata wa marekebisho ya mahakama ya utawala huo umeakhirishwa hadi mwezi ujao.
Shikma Bressler, mmoja wa viongozi wakuu wa vuguvugu la maandamano dhidi ya serikali ya Israel amesema: "Tutaendelea kuandamana mitaani kama mpango huo hautatupiliwa mbali kikamilifu."
Bressler amesema Netanyahu na washirika wake wamedhamiria kuendelea na "sheria zao za udikteta" katika kikao kijacho cha Knesset, ambacho kinatarajiwa kufanywa mwezi mmoja ujao.
Amesema marekebisho yaliyopendekezwa, ambayo yatapunguza mamlaka ya Mahakama ya Juu na kulipa Bunge la Israel (Knesset) mamlaka ya kubatilisha maamuzi ya Mahakama ya Juu, "yanadhuru. uchumi na usalama wa Israeli.”
Sambamba na hayo maandamano ya wazayuni waliokuwa na hasira yaliendelea huko Israel jana Jumanne licha ya uamuzi wa Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu, kusimamisha kwa muda mpango wake wenye utata wa kupunguza mamlaka ya Mahakama ya Juu.
Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel amelazimika kuakhirisha utekelezaji wa mpango wake wa kile kinachoitwa 'mageuzi ya mahakama' kufuatia maandamano ya Wazayuni dhidi ya mpango huo kwa wiki 12 mfululizo.
Katika hotuba yake aliyoitoa kwa njia ya televisheni siku ya Jumatatu baada ya maji kumfika shingoni kutokana na maandamano ya karibu miezi mitatu, Netanyahu alisema, "Nimeamua kuakhirisha usomaji (uwasilishaji) wa pili na wa tatu (wa muswada huo) ili tufikie mapatano mapana."
Machafuko na maandamano ya sasa huko Israel yamepelekea kuongeza maonyo kuhusu uwezekano wa kuibuka vita vya wenyewe kwa wenyewe miongoni mwa Wazayuni wanaokalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina.