Iraq yakaribisha taarifa ya pamoja ya Syria na Saudia
Apr 14, 2023 07:18 UTC
Iraq imekaribisha taarifa ya pamoja ya Syria na Saudi Arabia, iliyotolewa mwishoni mwa ziara ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Faisal al-Miqdad mjini Riyadh siku ya Jumatano.
Al-Maqdad na ujumbe alioandamana nao waliwasili Jeddah Jumatano jioni kwa safari ya kikazi kwa mwaliko wa waziri mwenzake wa Saudi Arabia Faisal bin Farhan ili kujadili na kubadilishana mawazo juu ya uhusiano wa pande mbili na masuala yanayopewa umuhimu wa pamoja.
Kwa mujibu wa ripoti ya shirika rasmi la habari la Syria (SANA) kutoka Baghdad, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq imetoa taarifa na kutangaza kuwa: Baghdad inatumai kuwa juhudi za Damascus na Riyadh zitasaidia kuimarisha mfungamano na mshikamano kati yao na kwamba ushirikiano huo utakuwa na manufaa kwa uchukuaji hatua za pamoja nchi za Kiarabu.
Katika taarifa hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq imeongeza kuwa: nchi hiyo inakaribisha juhudi zozote za kuutatua mgogoro wa Syria na inaunga mkono kwa dhati kuhitimishwa mgogoro huo kwa njia za amani.
Katika taarifa hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq imetangaza kuwa, haitasita kufanya juhudi zozote katika mchakato wa kuirejesha Syria katika nafasi yake ya Kiarabu na kushiriki katika kila juhudi zitakazopelekea kumalizika migogoro katika eneo.
Mwishoni mwa kikao cha Jumatano kilichofanyika mjini Jeddah, mawaziri wa mambo ya nje wa Syria na Saudi Arabia walitoa taarifa ya pamoja kwa vyombo vya habari ya kukaribisha kuanza kwa mchakato wa kurejesha huduma za kibalozi na safari za ndege kati ya nchi hizo mbili na kusisitiza umuhimu wa kuimarishwa usalama na kupambana na aina zote za ugaidi.
Mara baada ya kuanza mgogoro wa Syria mwaka 2011, serikali ya Saudi Arabia na baadhi ya nchi nyingine za Kiarabu zilijiweka kwenye safu ya mbele ya waungaji mkono wakuu wa makundi ya kigaidi yanayoipinga serikali ya Damascus na kuvunja uhusiano wao na Damascus kwa kufunga balozi zao nchini humo.../