Maandaano ya bendera na uwezekano wa kutokea vita vingine Palestina
Kwa mujibu wa kalenda ya Kiibrania, maandamano ya Siku ya Bendera yalifanyika jana Mei 18, maandamano ambayo ni nembo ya ubaguzi wa rangi wa utawala ghasibu wa Israel dhidi ya taifa la Palestina na jamii nyinginezo kwa ujumla.
Ni wazi kuwa utawala wa Kizayuni ni utawala uliojengeka katika msingi wa kukalia kwa mabavu ardhi za Wapalestina na kuendesha siasa za mabavu na ubaguzi wa rangi katika ardhi hizo. Kuna tabia na mienendo mingi ya utawala huo inayothibitisha wazi ubaguzi huo wa rangi. Maandamano ya bendera ambayo yalifanyika jana karibu na Msikiti wa al-Aqsa ni moja ya mienendo hiyo ya kibaguzi.
Baada ya kutangazwa uwepo wa utawala wa Kizayuni katika Siku ya Nakba Mei 14, 1948, eneo la magharibi mwa mji wa Quds lilitwaliwa kwa nguvu na utawala huo na eneo la mashariki likawekwa chini ya udhibiti wa Jordan. Lakini hatimaye, kufuatia vita vya siku sita kati ya Waarabu na utawala wa Kizayuni na ushindi wa utawala huo mwezi Juni 1967, sehemu ya mashariki nayo iliunganishwa na sehemu ya magharibi ya Quds (Jerusalem), tukio ambalo lilitokea tarehe 28 Ayar kwa mujibu wa kalenda ya Kiarabu yaani Mei 18. Tel Aviv huadhimisha siku hii kwa jina la "Siku ya Jerusalem" (Quds).
Katika siku hii sherehe za Wazayuni huambatana na ukatili mkubwa dhidi ya Wapalestina. Sababu kuu ni kwamba Wazayuni wanajaribu kubadilisha utambulisho wa Msikiti wa al-Aqswa na kutekeleza stratijia ya Uyahudi kuhusu msikiti huo mtakatifu ambao ni Kibla cha kwanza cha ulimwengu wa Kiislamu. Kuhusiana na hilo, mnamo tarehe 18 Mei, Wazayuni walipitia Bab al-Amoud na vitongoji vya kale vya Quds na kufika kwenye ua za Msikiti wa al-Aqswa, na kisha kufanya sherehe inayoitwa “Densi ya Bendera” ambapo walowezi wa Kizayuni, kupitia hatua hiyo ya kichochezi, wametaka kufukuzwa Wapalestina katika eneo la Quds.
Hii ni katika hali ambayo Wapalestina wanatilia mkazo kulindwa utambulisho wa Kiislamu wa Msikiti wa al-Aqswa na kupinga hatua za kibaguzi za Wazayuni katika eneo hilo takatifu. Jana asubuhi, jeshi la maghasibu wa Kizayuni lilitumwa katika eneo la mashariki mwa Msikiti wa al-Aqswa ambapo liliwafukuza Waislamu na kuandaa uwanja wa walowezi wa Kizayuni kuuvunjia heshima msikiti huo. Tofauti iliyoko kati ya maandamano ya bendera ya mwaka huu na ya miaka iliyopita ni kwamba kuna watu wenye itikadi kali na wabaguzi wa rangi katika baraza la mawaziri la sasa la Israel ambao wanaruhusu kufanyika vurugu na kutumika mabavu dhidi ya Wapalestina wasio na hatia. Kwa kuzingatia hayo, Jumuiya ya Kizayuni inayojulikana kwa jina la "Hekalu la Bidino" inajaribu kuwahamasisha watu 5,000 kuuvunjia heshima Msikiti wa al-Aqswa kwa kutumia uchochezi unaoendelezwa na mawaziri wenye itikadi kali katika baraza la mawaziri la Netanyahu.
Tofauti nyingine ya wazi ni kwamba utawala wa Kizayuni ndio kwanza umesitisha vita vya siku tano dhidi ya Ukanda wa Gaza. Ukaribu wa vita hivyo na maandamano ya Siku ya Bendera unamaanisha kuwa mizozo huwa haiko mbali na maadhimisho ya siku hii. Katika miaka ya nyuma pia maandamano hayo yaliambatana na mizozo na ghasia kubwa. Utawala wa Kizayuni umeugeuza mji wa Quds kuwa kambi ya kijeshi na umeweka zaidi ya askari 3,000 katika maeneo tofauti ya mji huo. Pia, polisi wa Israel wametumia zana zingine kama vile ndege zisizo na rubani na helikopta ili kukandamiza Wapalestina na kudhibiti hali ya mambo katika eneo hilo takatifu.
Ikiwa ni katika kujibu hatua za kichochezi za baraza la mawaziri la Netanyahu na maandamano ya bendera, chumba cha pamoja cha kuratibu masuala ya makundi ya mapambano ya Palestina kilitangaza kuwa: "Viongozi wa mapambano wanafuatilia kwa karibu hali ilivyo, tumetuma ujumbe wetu kwa wapatanishi ambao wanapaswa kuchukua hatua za lazima kabla ya muda kuisha ili kuzuia maandamano ya bendera. Uamuzi wetu uko wazi kabisa, hatujaurudisha Upamga wa Quds kwenye ala yake."