Wairaqi waandamana kumuunga mkono Sheikh Qassim wa Bahrain
Wananchi wa Iraq wamefanya maandamano ya kuonyesha uungaji mkono wao kwa mwanachuoni mkubwa wa Kiislamu Ayatullah Sheikh Isa Qassim ambaye hivi karibuni alivuliwa uraia na utawala wa Aal-Khalifa wa Bahrain.
Maandamano hayo ya jana Ijumaa yamefanyika katika mji mkuu Baghdad na mji wa Basra, ambapo waandamanaji wameilaani serikali ya Manama kumpokonya uraia Sheikh Qassim. Mamia ya waandamanaji waliokuwa wamebeba mabango yenye picha ya Sheikh Qassim pamoja na jumbe za kulaani hatua ya Manama kumpokonya uraia msomi huyo, walikusanyika nje ya ubalozi wa Bahrain katika wilaya ya Mansour, viungani mwa mji mkuu Baghdad na kupiga nara za kuitaka Bahrain iangalie upya uamuzi wake huo unaokanyaga sheria za kimataifa. Shughuli za usafiri katika eneo hilo zilitatizwa baada ya waandamanaji hao kufunga madaraja ya Jadriya na Shuhada katika maandamano hayo. Hapo jana Jumuiya ya Kimataifa ya Kukurubisha Madhehebu za Kiislamu imelaani hatua ya utawala wa Aal-Khalifa kumvua uraia mwanachuoni mashuhuri wa Kiislamu nchini Bahrain Ayatullah Sheikh Isa Qassim. Kamisheni Kuu ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni baadhi ya nchi na asasi za kimataifa zilizotoa taarifa ya kulaani kupokonywa uraia Ayatullah Qassim, kwa madai kuwa ametumia vibaya nafasi yake kwa maslahi ya madola ya kigeni.