Makundi ya muqawama Palestina: Tutalipiza kisasi cha mauaji ya Jenin
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i99514-makundi_ya_muqawama_palestina_tutalipiza_kisasi_cha_mauaji_ya_jenin
Makundi ya muqawama wa Palestina yameapa kuwa yatalipiza kisasi cha damu za Wapalestina waliouawa shahidi katika mashambulizi ya kinyama ya jeshi la utawala wa Kizayuni katika mji wa Jenin, eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
(last modified 2026-03-17T04:36:21+00:00 )
Jul 04, 2023 03:46 UTC
  • Makundi ya muqawama Palestina: Tutalipiza kisasi cha mauaji ya Jenin

Makundi ya muqawama wa Palestina yameapa kuwa yatalipiza kisasi cha damu za Wapalestina waliouawa shahidi katika mashambulizi ya kinyama ya jeshi la utawala wa Kizayuni katika mji wa Jenin, eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Katika taarifa iliyotolewa jana Jumatatu, mrengo wa muqawama huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu umesisitiza kuwa, hakuna shaka kuwa wanamuqawama watafanya operesheni za kulipiza kisasi jinai za utawala huo dhidi ya Wapalestina.

Taarifa hiyo imesema: Kambi ya Pamoja ya Makundi ya Muqawama wa Palestina imejiandaa kukabiliana na uvamizi wa kikatili wa Wazayuni dhidi ya Jenin. Muqawama umo katika kona zote na hautamruhusu adui ashambulie watu wetu Jenin.

Aidha Harakati ya Jihad Islami imetoa taarifa ikitangaza kuwa, adui Mzayuni ajiandae kwa vipigo kwa kuhusika kikamilifu na mauaji hayo ya kigaidi na kueleza kuwa, adui hatafikia malengo yake kwa jinai hiyo. 

Makundi ya muqawama na mapambano ya ukombozi wa Palestina yamesema yatafanya oparesheni za jibu la moja kwa moja kwa uvamizi mbaya zaidi wa kijeshi wa Israel katika mji wa Jenin, eneo la Ukingo wa Magharibi.

Jeshi la utawala wa Kizayuni jana Jumatatu lilifanya mashambulizi ya kinyama ya anga na kuushambulia mji wa Jenin huko kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, na kuua shahidi Wapalestina 11 na kujeruhi wengine zaidi  ya 50.

Ukatili wa Wazayuni mjini Jenin

Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu (OIC) imesema kuwa, maghasibu wa Israel wanahusika moja kwa moja na jinai hizo za kikatili ambazo zinapasa kuchunguzwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria.  

Kadhalika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu sanjari na kulaani vikali jinai hizo zinazotekelezwa na jeshi la utawala wa Kizayuni katika eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan, imeitisha kikao cha dharura leo Jumanne kuzungumzia uhalifu huo wa Wazayuni.