Muqawama wawapongeza Wapalestina kwa ushindi mkubwa Jenin
Makundi ya muqawama yamewapongeza wananchi wa Palestina kwa kupata ushindi mkubwa wa kufanikiwa kuzima uvamizi na mashambulizi ya jeshi katili la Israel dhidi ya Wapalestina katika mji wa Jenin, kaskazini mwa eneo la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.
Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amewapongeza Wapalestina kwa ushindi huo ambao umeudhalilisha na kuutweza utawala wa Kizayuni.
Operesheni hizo za wanamuqawama na mujahidina wa Kipalestina zimehitimisha uvamizi na hujuma za kinyama za jeshi la Israel na kuwalazimisha wanajeshi makatili wa Israel kuondoka kwa idhilali kwenye mji huo.
Ismail Haniya amebainisha kuwa, "Tunamwambia adui Mzayuni kwamba, siku za kufanya jinai dhidi ya taifa la Palestina pasi na kulipa gharama zimekwisha."
Naye Katibu Mkuu wa Harakati ya Jihadul Islami ya Palestina, Ziyad al-Nakhalah amepongeza ushindi huo wa taifa la palestina mkabala wa Wazayuni na kueleza kuwa, ushindi huo wenye izza umetokana na operesheni za Brigedi za Jenin kwa kushirikiana na Brigedi za al-Quds.
Amesisitiza kuwa, mujahidina wa Kipalestina hawapaswi kuwa na shaka wala kigugumizi katika vita na adui Mzayuni kwani adui huyo muda si mrefu ataangamia.
Jeshi la utawala wa Kizayuni tangu juzi Jumatatu limefanya mashambulizi ya kinyama ya anga na kuushambulia mji wa Jenin huko kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, na kuua shahidi Wapalestina 12 na kujeruhi makumi ya wengine.
Hata hivyo makundi ya muqawama wa Palestina yamefanya operesheni za kulipiza kisasi cha damu za Wapalestina waliouawa shahidi katika mashambulizi hayo ya kinyama, na kufanikiwa kuwatimua wanajeshi la utawala wa Kizayuni kutoka mji wa Jenin, kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.