Jul 23, 2023 02:18 UTC
  • China yalaani njama ya Ulaya ya kushamirisha

Mwakilishi wa China katika ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva amelaani kitendo kiovu kilichofanywa na Sweden na Denmark cha kuruhusu kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu na kusisitiza kuwa Beijing inapinga uenezaji chuki dhidi ya Uislamu.

Baada ya hatua iliyochukuliwa katika nchi za Sweden na Denmark ya kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu, Chen Xu, mwakilishi wa China katika ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva amelaani hatua yoyote inayochukuliwa kukivunjia heshima kitabu kitakatifu cha Waislamu.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, baada ya hatua zilizochukuliwa hivi karibuni barani Ulaya za kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu, Xu amesema: "Beijing inalaani vikali kuanza tena uchomaji moto wa Qur'ani na inaunga mkono mpango wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa kufuatia uchomaji moto wa Qur'ani uliofanywa nchini Sweden."
Akizihutubu nchi za Ulaya zinazotoa kibali cha kufanywa vitendo hivyo vya kishenzi kwa kisingizio cha kuunga mkono uhuru wa kutoa maoni, mwanadiplomasia huyo wa China amesema: 'uhuru wa kutoa maoni' usitumike kama kisingizio cha kuchochea mgongano kati ya staarabu.

Juzi Ijumaa, wanachama wa kundi moja la mrengo wa kulia lenye misimamo ya chuki linalojiita Danske Patrioter (Wazalendo wa Denmark) walikusanyika mbele ya ubalozi wa Iraq katika mji mkuu wa Denmark, Copenhaigen wakiwa wamebeba bendera zenye maandishi ya chuki dhidi ya Uislamu na kupiga makelele ya matusi dhidi ya Uislamu.

Harakati hiyo ya chuki dhidi ya Uislamu ilifanyika siku moja tu baada ya tukio la siku ya Alkhamisi Julai 20, ambapo kwa mara ya pili ndani ya muda wa wiki chache waliohusika na uchomaji moto wa Qur'ani nchini Sweden walikivunjia heshima tena kitabu hicho kitakatifu cha Waislamu katika mkusanyiko uliofanyika katika mji mkuu wa nchi hiyo Stockholm kwa kibali na ulinzi kamili wa Polisi.
Vitendo hivyo vya kuivunjia heshima Qur'ani vinavyofanywa katika nchi za Ulaya vimeibua mijibizo na kukabiliwa na hatua mbalimbali.
Mapema jana Jumamosi, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iraq alilaani kitendo cha kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu na bendera ya Iraq mbele ya ubalozi wa nchi hiyo nchini Denmark na kuitaka Jamii ya Kimataifa ichukue hatua ya kukabiliana na jinai hizo.
Kufuatia kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu barani Ulaya, Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa Jumatano ya wiki iliyopita lilipitisha azimio kuhusiana na chuki za kidini, na kumtaka Rais wa baraza hilo kutoa ripoti kuhusiana na chuki za kidini.
Azimio la Baraza la Haki za Kibinadamu la Umoja wa Mataifa pia limezitaka serikali kupitia upya sheria zao na kuchunguza vifungu vinavyotoa mianya ya kutodhibitiwa wala kufuatiliwa kisheria bali kuwaunga mkono wanaoeneza chuki za kidini.../

 

Tags