Aug 29, 2023 02:44 UTC
  • Wasiwasi wa UN juu ya kuwepo na kuongezeka harakati za DAESH (ISIS) nchini Afghanistan

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine tena limeelezea kwamba linatiwa wasiwasi na kuwepo na kuongezeka kwa shughuli za kundi la kigaidi la DAESH (ISIS) nchini Afghanistan.

Kwa mujibu wa mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, Afghanistan haipasi kuwa kimbilio salama kwa makundi ya kigaidi, yakiwemo Al-Qaeda na DAESH (ISIS). Vladimir Voronkov, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na mapambano dhidi ya ugaidi amesema katika mkutano wa Baraza la Usalama: "Hali ya usalama nchini Afghanistan ni mbaya; na mbali na ISIS, karibu makundi mengine 20 ya kigaidi yanaendesha harakati zao nchini Afghanistan. Hata hivyo, kundi la Taliban ambalo limerejea madarakani kwa mara ya pili nchini Afghanistan, lina mtazamo tofauti juu ya suala hilo likiamini kuwa moja ya mafanikio liliyopata katika miaka miwili iliyopita ni kuimarisha misingi ya usalama nchini Afghanistan.

Kuwepo kwa harakati za makundi ya kigaidi ya ISIS na al-Qaeda na makundi mengine 20 nchini Afghanistan si suala jipya kwa sababu maafisa wa serikali iliyopita ya nchi hiyo nao pia walilizungumzia jambo hilo mara kadhaa. Lakini nukta muhimu ni kwamba makundi hayo yalipanua wigo wa harakati zao katika miongo miwili ya Afghanistan kukaliwa kwa mabavu na Marekani na shirika la kijeshi la NATO, na sio jambo geni katika masuala ya usalama ya nchi hiyo.

Baraza la Usalama la UN

Kuhusiana na suala hilo, Matin Haidar, mtaalamu wa masuala ya Afghanistan anasema: "masuala ya usalama siku zote yamekuwa ndio udhaifu unaotumiwa na Marekani na washirika wake kuingilia masuala ya Afghanistan, na huwa wanayaibua kila mara kwa njia na mbinu mbalimbali, ikiwemo kulitumia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kuhusiana na harakati za kigaidi na vitisho vyao kwa Afghanistan na eneo kwa ujumla, hakuna shaka kuwa indhari iliyotolewa na Baraza la Usalama ni sahihi kabisa, lakini ingekuwa bora kama Baraza hilo lingechunguza kwanza chimbuko la uwepo wa magaidi nchini Afghanistan kisha likapanga na kutekeleza mpango madhubuti wa kuwatokomeza magaidi hao".

Russia pia imekuwa ikitoa tahadhari kila mara kuhusu kuongezeka kwa uwezo wa tawi la Khorasan la kundi la kigaidi la DAESH (ISIS) ndani ya Afghanistan. Kulingana na maelezo ya Moscow, kuwa tata zaidi mashambulizi yanayofanywa na Daesh dhidi ya Taliban na vituo vya kimataifa ni ishara kwamba uwezo wa kufanya hujuma za kigaidi wa kundi hilo lililowekewa vikwazo, umeongezeka ndani ya ardhi ya nchi hiyo.

Duru za usalama zinaamini kuwa, wanachama wa kundi la kigaidi la DAESH nchini Afghanistan ni mabaki ya magaidi walewale wa kundi hilo walioshindwa huko Syria, Afghanistan na hata Yemen, ambao wamehamishiwa na kuzatitiwa upya huko Afghanistan kwa msaada na ushirikiano wa Marekani. Kwa muktadha huo, baada ya Marekani na NATO kuondoka kimadhila katika ardhi ya Afghanistan, inaonekana kuwa, hivi sasa zimeamua kuibua masuala ya usalama ya nchi hiyo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hususan harakati za kundi la kigaidi la Daesh ili kujaribu kuandaa mazingira ya kurudi tena huko Afghanistan. Mortaza Hossein, mtaalamu wa masuala ya Afghanistan anasema kuhusiana na suala hilo: "Marekani na NATO ndizo sababu kuu ya kuendelea kukosekana amani na usalama Afghanistan wakati wa miongo miwili ya kuikalia kwa mabavu nchi hii. Na sababu ni kuwa kwa kuliunda kundi la Daesh, sio tu Marekani iliwaandaa na kuwazatiti wanachama wa kundi hilo ndani ya Afghanistan, lakini pia inadhamiria kuwatumia kimaslahi magaidi hao kwa ajili ya malengo yake ya baadaye. Kwa hivyo inavyoonekana, maonyo ya mtawalia yanayotolewa na Baraza la Usalama kuhusu masuala ya usalama nchini Afghanistan yanaandaa mazingira ya utekelezaji wa malengo ya nyuma ya pazia ya Marekani katika eneo na Afghanistan."

Alaa kulli haal, moja ya hatua iliyochukuliwa kwa mahesabu kamili na Marekani nchini Afghanistan ni kuacha silaha na zana mbalimbali za kivita, ikiwa inaaminika kuwa muhimu zaidi kati ya hizo zimeingia mikononi mwa makundi ya kigaidi yaliyoko nchini humo. Maria Zablotskaya, naibu mwakilishi wa Russia ambaye amehutubia kikao cha Baraza la Usalama, amekosoa kitendo cha Marekani kuacha silaha na zana za nchini Afghanistan na kusisitiza kuwa silaha hizo hivi sasa ziko mikononi mwa makundi ya kigaidi ya nchini humo na kwamba kuachwa kwa zana hizo kutahatarisha amani na usalama wa eneo.

Askari vamizi wa Marekani wakiondoka Afghanistan

Kabla ya hapo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitangaza katika ripoti yake kwamba kundi la Daesh limeongeza uwezo wake wa kivita nchini Afghanistan na idadi ya wapiganaji wa kundi hilo inakadiriwa kuwa kati ya elfu nne hadi sita. Na hii ni katika hali ambayo, kulingana na ripoti ya awali ya baraza hilo, idadi ya magaidi wa Daesh ilikuwa wanamgambo wapatao 3,500, hali ambayo inaonesha ongezeko kubwa kwa mtazamo wa kitakwimu. Kutokana na hali hiyo, inapasa nchi za eneo ziimarishe ushirikiano wao wa kiusalama ili ziweze kukabiliana kwa dhati na hatari zinazosababishwa na uwepo wa kundi la kigaidi la DAESH (ISIS) nchini Afghanistan; na kutoruhusu nchi za Magharibi zilitumie suala hilo kama fursa ya kurudi tena katika eneo na hasa Afghanistan…/

 

Tags