NYT: Ukuaji wa uchumi wa Russia utaupiku wa US na EU
Gazeti la New York Times limeripoti kuwa, uchumi wa Russia ni imara na madhubuti kinyume na matarajio ya serikali za Magharibi, ambazo zilitazamia uchumi huo utalemazwa kikamilifu na vikwazo vyao dhidi ya Moscow.
Kwa mujibu wa gazeti hilo la Marekani, vikwazo shadidi vya Wamagharibi dhidi ya Russia tangu vianze vita vya Ukraine, havijakuwa na matokeo mengine isipokuwa kuisukumu Russia itazame upya uchumi wake kupitia kupiga jeki uzalishaji na kuelekeza fedha nyingi katika sekta ya viwanda.
Gazeti la New York Times limenukuu makadirio ya Benki Kuu ya Russia yanayoonesha kuwa, mapato ya Russia yataimarika kwa asilimia 2.5 mwaka huu, na huenda yatapiku ya Umoja wa Ulaya na hata Marekani.
Kwa mujibu wa gazeti hilo la Marekani, sarafu ya ruble ya Russia ilikumbwa na mtikisiko katika msimu wa machipuo mwaka jana 2022 pekee, lakini baada ya hapo, thamani yake imeendelea kuimarika na kupata nguvu.
Kadhalika ripoti mpya ya Benki ya Dunia inaeleza kuwa, nchi wanachama wa kundi la BRICS ikiwemo Russia, zimezitumulia kivumbi nchi za kundi la G7 katika kiwango cha ushiriki kwenye ukuaji uchumi duniani.
Wataalamu wa uchumi wanasema kuwa, nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani hivi sasa zinahisi kikamilifu mabadiliko ya nguvu ya kimataifa kutoka Magharibi hadi Mashariki, na zinafanya mikakati ya kuzusha matatizo ili kuzusha migogoro ya kimataifa.