Ushirikiano wa Korea Kaskazini na Russia dhidi ya Marekani
Katika mazungumzo yake na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, Sergei Lavrov, Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia, wamejadiliana kuhusu uhusiano wa pande mbili na ushirikiano wao wa hivi sasa na kusisitiza juu ya makubaliano yao ya kutatua kidiplomasia masuala yenye utata katika Peninsula ya Korea.
Pande hizo mbili pia zimetangaza azma yao ya kukabiliana na siasa za kujitanua za Marekani, ambazo zinahatarisha eneo zima la Asia-Pacifiki.
Inaonekana kuwa kuna umuhimu wa kuimarishwa ushirikiano kati ya Moscow na Pyongyang wakati Russia iko vitani na Ukraine na wakati huo huo Marekani inazidisha mashinikizo yake dhidi ya Russia na Korea Kaskazini,
Mtaalamu wa masuala ya kisiasa Lee T-Wan anasema kuhusu jambo hilo kuwa Marekani haikufikiria kwamba Korea Kaskazini, Russia na hata China zingeweza kutatua baadhi ya tofauti zilizopo na kuboresha uhusiano wao hasa kuhusiana na mgogoro wa Ukraine, suala ambalo limepelekea nchi za Magharibi kuwa na wasiwasi kuhusiana na kiwango cha uhusiano wa Russia, China na Korea Kaskazini.
Wakati huo huo, tishio la Korea Kaskazini dhidi ya Marekani la kufanya mashambulizi ya mapema katika kukabiliana na hatari ya kutumwa zana za kijeshi za Marekani katika eneo hilo ikiwemo ndege ya kivita ya kudondosha mabomu ya nyuklia aina ya B-52, linaonyesha kuwa Korea Kaskazini si tu kwamba imejiandaa vilivyo kukabiliana na mashambulizi ya aina yoyote ile ya Marekani na waitifaki wake wa eneo bali pia inaweza kuanzisha mashambulizi ya mapema ili kujilinda kutokana na mashambulizi ya aina yoyote ya Marekani.

Kwa mtazamo wa Korea Kaskazini, Marekani inafahamu vyema kwamba eneo la Peninsula ya Korea liko katika hali ya vita na zana za kivita zinazopelekwa katika nchi waitifaki wake zitakuwa za kwanza kulengwa wakati wa makabiliano. Hilo ni onyo muhimu kwa Japan na Korea Kusini ambazo katika miaka ya hivi karibuni zimeimarisha mwenendo wa kujirundikia zana za kijeshi na kuweka zana za jeshi la Marekani katika ardhi zao.
Wen Ti Song, mhadhiri wa taaluma ya siasa katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Australia ambaye pia ni mtaalamu wa masuala ya kimataifa, anasema kuhusiana na jambo hilo kuwa: Katika miaka ya hivi karibuni, Marekani imekuwa ikifuatilia siasa za kuimarisha zana zake za kisasa kama vile makombora ya THAAD, nchini Korea Kusini. jambo ambalo limezitia wasiwasi nchi za Korea Kaskazini na China. Kwa hiyo, onyo la Korea Kaskazini kwa Marekani kuhusiana na siasa zake za kijeshi huko Asia Mashariki pia linaweza kuwa tishio kubwa kwa washirika wake.
Kwa vyovyote vile, kwa mtazamo wa duru za kieneo, zikiwemo za Korea Kaskazini, zama za Marekani kuhodhi fursa za kuanzisha mashambulizi zimepitwa na wakati, hivyo kutua ndege za kubeba mabomu ya nyuklia, aina ya B-52 na za kizazi kipya cha tano za F-22 kusini mwa Peninsula ya Korea kunahesabiwa na Korea Kaskazini kuwa tishio kubwa kwa usalama wake wa kitaifa.

Kwa vyo vyote vile, kutia nanga manowari ya kubeba ndege za nyuklia ya USS Ronald Reagan katika bandari ya Busan, iliyoko kusini-mashariki mwa Korea Kusini, kwa muda wa siku tano, kufuatia manova za kijeshi za nchi tatu za Marekani, Japan na Korea Kusini, kunaonyesha wazi kuwa Washington bado inafuatilia mwenendo wa kuimarisha muungano wa kijeshi na waitifaki wake wa kikanda dhidi ya Korea Kaskazini, China na hata Russia.
Kwa mujibu wa Kim Tungmyung, mtafiti wa siasa za kimataifa wa Korea Kaskazini, zana za nyuklia za Marekani ni zaidi ya tisho linalodaiwa na nchi hiyo katika eneo la Peninsula ya Korea, na hatua hiyo ya kichochezi, imeugeuza ulimwengu mzima kuwa uwanja uliojaa hatari ya milipuko ya nyuklia. Ni kwa ajili hiyo ndiyo, kiongozi wa Korea Kaskazini akatilia mkazo katika mazungumzo yake na waziri wa mambo ya nje wa Russia kwamba Pyongyang iko tayari kabisa kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kati yake na Rais Vladimir Putin katika safari yake ya hivi karibuni nchini Russia.