Kuadhibiwa waungaji mkono wa Palestina katika vyuo vikuu vya Marekani
(last modified Mon, 13 Nov 2023 02:47:29 GMT )
Nov 13, 2023 02:47 UTC
  • Kuadhibiwa waungaji mkono wa Palestina katika vyuo vikuu vya Marekani

Licha ya madai ya kuheshimiwa uhuru wa kujieleza katika nchi za Magharibi ikiwemo Marekani, lakini ukweli wa mambo ni kwamba kuna mistari miekundu katika uwanja huo, likiwemo suala la kutetea kadhia ya Palestina, ambapo waungaji mkono wa taifa hilo linalodhulumiwa hukabiliwa na vikwazo vya aina mbalimbali vikiwemo vya kuadhibiwa na kufungwa jela.

Suala hilo limeshahidi hasa baada ya kutekelezwa operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa na kisha kufuatiwa na vita vya Gaza ambapo maelfu ya Wapalestina wanateswa na kuuliwa kinyama na utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza.

Kuhusiana na hilo, Chuo Kikuu cha Columbia kimetangaza kuwa kimesimamisha masomo kwa makundi mawili ya wanachuoi ambao waliongoza maandamano ya kutaka kusitishwa  vita huko Gaza.

Gerald Rosberg, Naibu wa chuo kikuu hicho maarufu, ametangaza katika taarifa ya eti kulinda usalama wa chuo hicho kuwa amesimamisha masomo kwa makundi mawili ya Students for Justice in Palestine SJP na Sauti ya Mayahudi kwa ajili ya Amani au Jewish Voice for Peace JVP hadi mwisho wa muhula Desemba 31. Mamia ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Columbia tarehe 9 Novemba walifanya maandamano yaliyoandaliwa na makundi hayo mawili na kuitaka Washington kuunga mkono usitishaji vita huko Gaza. Makundi yote mawili yana wafuasi katika mabweni mengi nchini na yameongoza maandamano dhidi ya sera za Washington na Tel Aviv.

Mauaji ya umati ya utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina

Jambo la kushangaza ni kwamba wafadhili wengi wa vyuo vikuu vya Marekani wanajiepusha kutoa michango yao ya mamilioni ya dola  kwa vyuo vya nchi hiyo kufuatia operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa na uungaji mkono wa baadhi ya wanachuo na wanafunzi wa Marekani kwa watu wa Gaza. Inasemekana kuwa sababu ya hatua hiyo ni kuadhibiwa vyuo vikuu vya Marekani ambavyo wanachuo wao wanaunga mkono mashambulizi ya vikosi vya wanamapambano wa Hamas dhidi ya Israel, kubana uhuru wa kujieleza na kuwajibishwa viongozi wa vyuo vikuu hivyo. Hii ni pamoja na kuwa wanafunzi ambao wanawaunga mkono Wapalestina na kukosoa hatua za utawala haramu wa Israel katika uwanja huo wanaadhibiwa.

Mgogoro kati ya utawala wa Kizayuni na makundi ya muqawama ya Palestina umekuwa ukijadiliwa kwa muda mrefu nchini Marekani hasa katika vyuo vikuu vya nchi hiyo, ambavyo ni uwanja wa kujadiliwa masuala ya kisiasa. Lakini kufuatia operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa na mashambulizi makali ya Israel ambayo yalikuwa hayajawahi kushuhudiwa tena huko nyuma katika Ukanda wa Gaza yameongeza sana mivutano na kudhihirisha wazi pengo kubwa la kisiasa na kijamii lililopo nchini Marekani, hasa katika mazingira ya vyuo vikuu. Makumi ya vyuo vikuu vya Marekani vimeathirika na hujuma ya kinyama ya utawala wa Kizayuni na mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina, na jambo hilo limepelekea wanafunzi katika vyuo vikuu kadhaa vya Marekani kufanya maandamano ya kulalamikia suala hilo.

Jumuiya 33 za makundi ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Harvard huko Marekani zilitia saini taarifa ya kushikamana na watu wa Gaza siku kumi baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa, na kuitaka Israeli kuwajibika kuhusiana na mashambulio dhidi ya Hamas. Taarifa hiyo ilisema: Matukio ya leo hayatokei bure. Kwa miongo miwili iliyopita, mamilioni ya Wapalestina huko Gaza wamelazimishwa kuishi katika gereza la wazi. Kwa miaka 75 sasa, mgogoro wa Israel umechukua sura tofauti, kuanzia kuporwa ardhi za Wapalestina, kuuawa kinyama kupitia mashambulio ya anga, kukamatwa kiholela katika vituo vya ukaguzi barabarani, kulazimishwa kutengana na familia zao hadi mauaji ya umati yanayotekelezwa kwa malengo maalumu.

Zareen Grewal, mhadhiri wa utafiti wa masuala ya Marekani katika Chuo Kikuu cha Yale, ameandika katika mtandao wa kijamii kama ifuatavyo: Israel ni taifa vamizi na katili, na Wapalestina wana haki ya kutumia silaha katika mapigano yao ya kujikomboa.

Jemma DeCristo, mhadhiri wa utafiti wa masuala ya Marekani katika Chuo Kikuu cha California, pia kwenye ujumbe wake kupitia mtandao wa kijamii wa X amewatuhumu waandishi wa habari wa Kizayuni kwa kusema uwongo na kuandika kwamba wanachapisha habari za hadaa. Misimamo hiyo imepelekea wahadhiri wawili hao kuadhibiwa.

Uungaji mkono mkubwa wa kimataifa kwa taifa la Palestina

Kuchukuliwa hatua kali za kidhalimu wanachuo, taasisi za kielimu na  wahadhiri wa vyuo vikuu wanaoikosoa Israel nchini Marekani kutokana na uungaji mkono wao kwa Wapalestina kwa mara nyingine tena kumefichua madai ya uongo ya nchi za Magharibi hususan Marekani kuhusu suala zima la eti kuheshimiwa haki za binadamu na uhuru wa kujieleza katika nchi hizo. Sera na siasa za undumakuwili za nchi za Magharibi hususan Marekani kuhusiana na uhuru wa kisiasa na  kujieleza zinaonesha wazi kuwa suala hilo hupewa umuhimu tu pale linapogusa masuala yanayofuatiliwa na Wamagharibi kama vile ya kuenezwa chuki dhidi ya Uislamu na kutusiwa matukufu ya Waislamu. La sivyo, kuzungumzia masuala mengine kama vile madai ya maangamizi ya Mayahudi na kutilia shaka vitendo vya jinai vya utawala wa Kizayuni na kuwaunga mkono Wapalestina na kadhia ya Palestina, hukabiliwa na jibu kali, mateso, vitisho na kukandamizwa na nchi hizo hizo zinazodai kutetea haki za binadamu na uhuru wa kujieleza. Masuala hayo yanathibitisha wazi kuwa huko Marekani ambako kuna lobi zenye nguvu za Wazayuni ambazo huzilazimisha pia Ikulu ya White House na Kongresi ya Marekani kujidhalilisha mbele ya utawala wa Kizayuni, hatua na harakati zozote za kupinga Wazayuni na kuwaunga mkono Wapalestina wanaodhulumiwa, ikiwemo katika vyuo vikuu, huhesabiwa kuwa dhambi kubwa isiyosameheka, ambayo hupelekea wanaoitenda kupata mateso makali na kuwekewa vikwazo vya kila aina.

 

Tags