Dec 01, 2023 07:59 UTC
  • Onyo la Moscow kuhusu kuendelea vita vya Ukraine mwaka 2024

Licha ya kupita karibu miezi 22 tangu kuanza vita vya umwagaji damu nchini Ukraine, lakini hakuna matumaini yoyote yanayoashiria kumalizika mzozo huo hivi karibuni. Hii ni katika hali ambayo nchi za Magharibi kwa sasa zimeshughulishwa na vita vya Gaza na hivyo kutozingatia sana vita vya Ukraine, jambo ambalo limeipelekea serikali yenye mielekeo ya Kimagharibi ya Kyiv kukata tamaa kuhusu kupata misaada zaidi ya nchi hizo.

Sergei Ryabkov, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia alisema Jumatano, Novemba 29, kwamba hakuna uwezekano wa kusitishwa  mapigano nchini Ukraine mwakani kutokana na msimamo ya nchi wa Magharibi, ambao haikubaliki kabisa na Moscow. Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Russia amefafanua maoni yake hayo kuhusiana na uhusiano wa Russia na NATO na vilevile Ukraine katika hali ambayo vyombo vya habari vya Magharibi vinadai kuwa  Marekani inafanya juhudi za kumaliza vita hivyo. Ryabkov amesema: Kwa bahati mbaya, Marekani inaongoza kundi ambalo linaendelea kukariri mpango wa amani uliopendekezwa na Zelensky na kudai kuwa ndio msingi unaoweza kuleta wa amani.

Mpango huo wa amani uliopendekezwa na Rais Volodymyr Zelenskyi wa Ukraine unataka pamoja na mambo mengine kurejeshwa ardhi za nchi hiyo zilizotekwa na Russia hadi kwenye mipaka yake ya kabla ya 2014, kupata fidia za vita kutoka Moscow na kushtakiwa maafisa wa Russia katika mahakama za kimataifa. Moscow imepinga mpango huo na kusema si wa kimantiki.

Kwa kuzingatia kushindwa mashambulizi ya kukomboa ardhi ya Ukraine, ambayo yalianza katikati ya 2023 katika medani tofauti za vita, malengo ambayo yamekuwa yakifuatiliwa na nchi za Magharibi hayajafikiwa hivyo nchi hizo zimekuwa zikijaribu kuishawishi Ukaraine ikubali katika mchakato wa kusitisha mapigano na Russia na kutia saini makubaliano ya amani.

Zana za kijeshi za Ukraine

Inaonekana kuwa waitifaki wa Magharibi wa Ukraine wanazingatia suala la kufanyika mazungumzo ya amani na Russia, kwa maslahi ya serikali ya Kyiv. Kuhusiana na suala hilo, Marekani na Ujerumani zinafanya juhudi za siri za kumshurutisha Rais Volodymyr Zelensky  wa Ukraine afanye mazungumzo na Russia.

Maafisa wakuu wa Ukraine, akiwemo Zelensky mwenyewe, hivi karibuni walikiri kwamba kushindwa mashambulizi ya vikosi vya Ukraine kufikia malengo yaliyokusudiwa kumepelekea kukata tamaa nchi za Magharibi kuhusu suala zima la kutuma misaada nchini humo. Suala hilo limeifanya Kyiv kutambua kwamba haiwezi kurejesha ardhi yake inayokaliwa na Russia. Wiki chache zilizopita, Josep Borrell, mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya alionya kwamba huenda misaada ya Marekani kwa Ukraine ikapungua na kuongeza kuwa Wanachama wa umoja huo wanapaswa kujiandaa kisiasa ili kufidia upungufu huo. Licha ya ukweli huo na kutokuwa tayari tena nchi za Magharibi kuendelea kutoa misaada ya kijeshi na silaha kama ilivyokuwa awali, lakini viongozi wa Ukraine wanakataa kufanya mazungumzo ya amani na Russia.

Kyiv imekuwa ikisisitiza mara kwa mara kwamba misaada ya silaha ya washirika wa Magharibi, ambayo imekuwa ikiongezeka tangu kuanza  vita vya Russia na Ukraine, ina umuhimu mkubwa kwa jeshi la nchi hiyo. Kwa hivyo viongozi wa Ukraine wanasisitiza juu ya kupewa misaada zaidi na zana za kisasa zaidi na nchi za Magharibi.

Hii ni katika hali ambayo baada ya operesheni ya Kimbunga cha Al-Aqsa na vita vya Gaza, Zelensky amekuwa akielezea wasiwasi wake kwamba, licha ya ahadi za washirika wake hao, misaada ya Magharibi kwa Kyiv imepungua sana.

Kukiri  rais wa Ukraine juu ya nafasi muhimu ya misaada ya nchi za Magharibi, zikiongozwa na Marekani, katika kuendelea vita vya Ukraine na Russia na uwezekano wa kulazimika Kyiv kujiondoa katika vita iwapo misaada hiyo itasimamishwa, kunaonyesha mchango mkubwa wa  nchi za Magharibi katika kuendeleza vita vya umwagaji damu nchini Ukraine, ambavyo sasa viko katika mwezi wake wa 22.

Marekani ikiwa kinara wa kambi ya Magharibi na NATO, imefanya kila jitihada za kuendeleza  vita vya Ukraine kwa lengo la kuidhoofisha Russia kadiri inavyowezekana na kuwasababishia wananchi wa nchi hiyo hasara kubwa. Viongozi wa Marekani na NATO wanaamini kwamba ushindi wa Russia katika vita vya Ukraine, utakuwa na maana ya kudhoofishwa nafasi ya jumuia hiyo ya kijeshi na kuimarika ushawishi wa kieneo na kimataifa wa Russia, na vilevile kubadilika kikamilifu mfumo wa kiusalama, kijeshi na kisiasa katika Ulaya kwa madhara ya nchi za Magharibi.

Kuhusiana na hilo, Jens Stoltenberg, Katibu Mkuu wa NATO,alisisitiza katika msimamo wake hivi karibuni nafasi muhimu ya umoja huo katika kuainisha uwiano wa kisiasa kati ya Russia na Marekani kuhusiana na vita vya Ukraine. Stoltenberg alisema  Jumatano: kushindi  kijeshi  Russia katika vita vya Ukraine kunaweza kudhoofisha nafasi ya Washington duniani

Tags