Umoja wa Mataifa wataka kuundwa Mahakama maalumu ya vita vya Gaza
Huku mashambulizi na mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni wa Israel yakiendelea Gaza, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu ametoa wito wa kuundwa mahakama maalumu kuhusiana na vita hivyo.
Martin Griffiths, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika Masuala ya Kibinadamu, amesema kwamba ukiukaji wa sheria katika vita vya Gaza unaonekana wazi na kuwa kuna haja ya kuanzishwa mahakama maalumu kuhusiana na jambo hilo.
Aidha amesisitiza kuwa idadi ya wahanga wa magonjwa mbalimbali inaweza kuwa kubwa mara kadhaa kuliko idadi ya vifo vya mashambuilizi ya mabomu katika Ukanda wa Gaza, na kuwa inatarajiwa kwamba idadi hiyo itaongezeka kwa kuanza kuondolewa uchafu wa mabaki ya mashambulizi hayo.
Kabla ya kuanza vita vya Gaza, kila siku lori 500 za misaada zilikuwa zikiingia ukanda huo kupitia vivuko tofauti. Siku moja kabla ya mahojiano hayo, lori 100 za misaada ziliingia Gaza kupitia kivuko cha Rafah kwenye mpaka na Misri. Kivuko hicho hakina uwezo wa kusimamia malori zaidi.
Utawala wa Kizayuni umekuwa ukiendesha vita vya kikatili katika Ukanda wa Gaza tokea tarehe 7 Oktoba, vita ambavyo kwa mujibu wa maafisa wa Palestina na duru za Umoja wa Mataifa, mbali na kusababisha maafa ya kibinadamu ambayo hayajawahi kushuhudiwa, vimeharibu miundombinu mingi na kuua shahidi maelfu ya raia, wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake.
Utawala huo ghasibu bado unaendeleza hujuma zake hizo katika maeneo yote ya Ukanda wa Gaza kwa siku ya 74, ambapo kufikia sasa watu 19,400 wameuawa shahidi na zaidi ya wengine 52,200 wamejeruhiwa.