Dec 26, 2023 07:00 UTC
  • Russia: Bila usitishwaji vita azimio la Baraza la Usalama halitakuwa kwa manufaa ya Gaza

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imetangaza katika taarifa kwamba azimio la hivi karibuni la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu Ukanda wa Gaza halitaathiri hali ya ukanda huo, na kwamba kuna udharura wa kutekelezwa usitishaji vita katika ukanda huo haraka iwezekanavyo.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia imesema katika taarifa hiyo kwamba, azimio nambari 2720 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa haliwezi kubadilisha hali ya Ukanda wa Gaza bila ya kusimamishwa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika ukanda huo. Imesema, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na wakuu wa mashirika ya kibinadamu wameeleza mara kadhaa kutokuwa rahisi kufikishwa misaada ya kibinadamu huko Gaza ambako utawala ghasibu wa Israel unaendeleza mashambulio makali na ya kinyama dhidi ya wakazi wa eneo hilo.

Kikao cha Baraza la Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa Ijumaa jioni lilipasisha azimio linalotaka kuongezwa haraka misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Wanachama 13 wa Baraza la Usalama waliunga mkono azimio hilo, huku Russia na Marekani zikijizuia kupiga kura.

Rasimu ya awali ya azimio lililopendekezwa na UAE kuhusu usitishaji mapigano wa kibinadamu katika Ukanda wa Gaza iliahirishwa wiki iliyopita kutokana na tishio la Marekani la kuipinga kwa kura ya veto na azimio lililopitishwa karibuni kwa hakika ni azimio lililobadilishwa madhumuni yake kwa maslahi ya utawala haramu wa Israel.

Tags