Umoja wa Mataifa: Vita vya Gaza lazima vikomeshwe
https://parstoday.ir/sw/news/world-i106928-umoja_wa_mataifa_vita_vya_gaza_lazima_vikomeshwe
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Masuala ya Kibinadamu Martin Griffiths amesema ni lazima Jamii ya Kimataifa itumie "ushawishi wake wote" kumaliza vita katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jan 07, 2024 07:44 UTC
  • Umoja wa Mataifa: Vita vya Gaza lazima vikomeshwe

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na Masuala ya Kibinadamu Martin Griffiths amesema ni lazima Jamii ya Kimataifa itumie "ushawishi wake wote" kumaliza vita katika Ukanda wa Gaza.

Griffiths amebainisha kuwa, mapigano ya siku 90 yamelifanya eneo hilo la Palestina "lisilowezekana kukaliwa na watu," na kwamba watu wa Gaza wanakabiliwa na vitisho vya kila siku dhidi ya uwepo wao.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema, makumi ya maelfu ya Wapalestina wameuawa au kujeruhiwa, huku maeneo waliyoambiwa wahamie kwa ajili ya usalama "yakikumbwa na mashambulizi ya mabomu," na kusisitiza kwamba haya yote yanatokea "huku dunia ikiwa inatazama tu."

"Gaza imetuonyesha ubaya mkubwa zaidi wa ubinadamu," amesema Griffiths na kusisitiza kuwa utumiaji nguvu za kijeshi hauwezi kutatua tofauti.

Martin Griffiths

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayehusika na masuala ya kibinadamu ameeleza kuwa, maafa ya afya ya umma yanatokea huko Gaza akitoa mfano wa kuenea kwa magonjwa ya kuambukiza katika makazi yenye msongamano wa watu katika eneo hilo huku mabomba ya maji taka yakifurika.

Griffiths amesema: "takribani wanawake 180 wa Kipalestina wanajifungua kila siku katika machafuko haya," na watoto wa Gaza hawana chochote zaidi ya kusikia "sauti za kutisha za vita". 

Amesisitiza kuwa, ni wakati wa pande husika kutimiza wajibu wao wote chini ya sheria ya kimataifa kwa kulinda raia na kuwaachilia mateka huku akiwatolea wito viongozi wa dunia kutumia ushawishi wao wote kuhakikisha hilo linatokea.../