Jan 13, 2024 02:47 UTC
  • Ombi la serikali ya China kwa watu wa Taiwan

Serikali ya China imewataka watu wa kisiwa cha Taiwan kutompigia kura William Lai, mgombea mkuu wa uchaguzi wa urais katika kisiwa hicho.

Uchaguzi mkuu unafanyika katika kisiwa hicho leo Jumamosi, Januari 13. China inaamini kuwa ushindi wake utaiongoza Taiwan katika njia ya makabiliano ya kijeshi. Kisiwa cha Taiwan kina wakazi milioni 23. China inakichukulia kisiwa hicho kuwa jimbo lililojitenga, na hivi karibuni Rais Xi Jinping wa China alisisitiza kwamba hatimaye kisiwa cha Taiwan kitakuwa chini ya udhibiti wa Beijing na kujiunga na ardhi mama ya China. Ushindi wa William Lai katika uchaguzi wa rais wa kisiwa cha Taiwan unaitia wasiwasi mkubwa serikali ya Beijing kwa sababu ni mtu anayepigania kujitenga kisiwa hicho, ambapo anaungwa mkono katika hilo na nchi za Magharibi hususan Marekani. Kwa kutilia maanani kuwa Taiwan inatumiwa na Marekani kama chombo cha kutoa mashinikizo dhidi ya serikali ya China, Beijing imeionya mara kwa mara Washington kuhusu matokeo hasi ya kuimarisha uhusiano na mrengo unaounga mkono kujitenga Taiwan.

Henry Kissinger, mchambuzi mkuu wa masuala ya kimataifa wa Marekani aliyeaga dunia karibuni, pia alikuwa ameionya Washington kuhusu kuvuka mstari mwekundu wa China kuhusiana na suala hilo. Lee T Wan, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema kuhusu jambo hilo: "China imekuwa ikiionya Marekani mara kwa mara kwamba Taiwan ni mstari mwekundu wa ardhi yake na kwamba kamwe haitalegeza msimamo kuhusu jambo hilo. Hata kama Marekani daima imekuwa ikitangaza kwa maneno matupu kuwa inatekeleza ahadi yake ya kuheshimu China moja, lakini kivitendo imekuwa ikifanya mambo kinyume na ahadi hiyo." Kwa hiyo, Mao Ning, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China, katika mkesha wa uchaguzi wa Taiwan, ameitaka Marekani kusitisha mawasiliano rasmi na Taiwan na pia kukomesha uingiliaji wake katika uchaguzi wa kisiwa hicho, na wakati huohuo kuionya Washington kuhusu matokeo hasi ya tabia hiyo.

Mao Ning, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China

China imesisitiza mara kwa mara kuwa inapinga vikali maingiliano yoyote rasmi kati ya Marekani na Taiwan, na kuwa wajumbe wa Bunge la Marekani wanapaswa kufuata kanuni ya China moja na kutambua vifungu vya mkataba wa pamoja wa Marekani na China. Wakati huo huo, kutokana na wasiwasi wa kuimarika nafasi ya China na kudhoofika satwa ya Marekani katika ngazi za kimataifa, tangu urais wa Barack Obama, Washington imekuwa ikitekeleza siasa za kudhibiti na kuizingira China kisiasa, kijeshi, kiuchumi na kiteknolojia. Mbali na kutuma meli za kivita za Marekani kwenye maji ya pembezoni mwa Uchina na kuunda muungano wa kuidhibiti Beijing, Washington pia inaunga mkono harakati za vyama vinavyotaka kuitenga Taiwan, kikiwemo chama tawala cha Democratic Progressive Party.

Li Song Zhuhua, mtaalamu wa masuala ya kimataifa anasema kuhusu hilo: Siasa za Marekani ni kuishughulisha China na masuala tofauti yakiwemo ya Taiwan. Kwa hakika siasa za Marekani ni kuiburuza China katika mashindano ya silaha na wakati huo huo kuongeza mizozo kati yake na Taiwan kwa kuunga mkono harakati za kukitenga kisiwa hicho, siasa ambazo hadi sasa zimeshindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa dhidi ya Beijing.

Kwa vyovyote vile, kushindwa chama tawala cha Democratic Progressive Party katika uchaguzi wa serikali za mitaa kumedhihirisha kwamba watu wa kisiwa cha Taiwan wanapinga vita na migogoro na kuchochewa mivutano na China, mivutano ambayo chama hicho kinaifuatilia kwa sasa. Suala hilo limeipa serikali ya China matumaini kuwa kwa kuwaonya watu wa Taiwan kuhusiana na matokeo mabaya ya siasa za kuibua mivutano zinazofuatiliwa na chama hicho tawala, itafanikiwa kuwashawishi Wataiwan wapige kura zao kwa makini na kumchagua mtu ambaye atafuata mkondo wa kuimarisha ushirikiano na maingiliano na China. Hii ni kwa sababu Marekani inatoa ishara zisizo sahihi na za kuwachanganya wapiga kura wa Taiwan, jambo ambalo linaweza kuwa na matokeo yasiyoweza kufidika kwa watu wa Taiwan na Taiwan yenyewe. Hata hivyo, chama tawala cha Democratic Progressive Party kinatarajia kuwa uungaji mkono wa Marekani na hitilafu zilizopo kati ya Washington na Beijing zitakuwa kwa manufaa yake na hatimaye kukipelekea kushinda uchaguzi huo.

Tags