Malaysia: Magharibi ni mshirika wa jinai za Israel kwa kimya chake
Waziri Mkuu wa Malaysia amezikosoa vikali nchi za Magharibi kwa kuendelea kufumbia macho matukio ya Gaza na kusisitiza kuwa, Wamagharibi ni washirika wa jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina kwa kimya chao hicho.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Anwar Ibrahim, Waziri Mkuu wa Malaysia akisema hayo katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X na kuongeza kuwa, licha ya asilimia kubwa ya jamii ya kimataifa kulaani jinai za Israel katika Ukanda wa Gaza, lakini mataifa ya Magharibi yameendelea kuidhihirishia dunia dhati na uhalisia wao kwa kunyamazia kimya mashambulizi hayo ya kinyama ya Wazayuni.
Waziri Mkuu wa Malaysia ameeleza bayana kuwa, wimbi la mauaji yanayoshuhudiwa hivi sasa Gaza, ni muendelezo wa jinai ambazo utawala huo wa Kizayuni umekuwa ukiwafanyia Wapalestina kwa zaidi ya miongo saba sasa.
Asilimia kubwa ya wananchi wa Malaysia ni Waislamu. Nchi hiyo haina uhusiano wa kidiplomasia ya utawala wa Kizayuni. Mara kwa mara imekuwa ikilaani jinai zinazofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina.
Malaysia imetoa msaada wa mamilioni ya dola kwa Gaza, na Waziri Mkuu wa nchi hiyo yuko mstari wa mbele katika kulaani jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina na ambazo zinaendelea hadi hivi sasa tangu tarehe 7 Oktoba, 2023.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, Malaysia ilipiga marufuku meli zote zenye bendera ya Israel kutia nanga kwenye bandari zake, ikiwa ni sehemu ya hatua za kulalamikia kivitendo jinai za utawala wa Kizayuni kwenye Ukanda wa Gaza na kuilaani Israel kwa kukiuka sheria za kimataifa kupitia mauaji na kikatili inayowafanyia Wapalestina.
Kadhalika Waziri Mkuu wa Malaysia amepongeza hatua ya Afrika Kusini ya kuishtaki Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kutokana na jinai za utawala huo katika Ukanda wa Gaza.