Jan 25, 2024 03:26 UTC
  • Rais wa UEFA: Kushiriki Israel na Ukraine mechi za EURO 2024 ni hatari kwa usalama

Rais wa Muungano wa Mashirikisho ya Soka ya Ulaya (UEFA) amesema kushiriki Israel na Ukraine katika fainali zijazo za michuano ya EURO 2024 ni hatari kwa usalama.

Aleksander Ceferin, Rais wa UEFA ameiambia Telegraph Sports kuwa, kushiriki Israel na Ukraine kwenye mechi za EURO 2024 kunaweza kuwa tishio la usalama kwa mashindano hayo ya kieneo yanayotazamiwa kufanyika katika msimu wa joto kali nchini Ujerumani.

Caferin ameeleza bayana kuwa, "Katika nyakati hizi za kiwendawazimu, ambapo kijiopolitiki dunia imewehuka, wasi wasi mkubwa uliopo ni masuala ya usalama."

Ameendelea kusema: Hofu yangu si tu viwanjani, kwa kuwa naamini viwanja vitapewa ulinzi wa kutosha, lakini mashabiki wa kila aina watazagaa kote kwenye majiji na miji (ya Ujerumani).

Rais wa UEFA ametoa indhari hiyo katika hali ambayo, chuki dhidi ya Wazayuni zimeongezeka kote duniani kufuatia vita vya utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Maandamano ya kupinga vita vya Gaza mjini Berlin

Maandamano ya kulaani jinai hizo za Israel huko Gaza yamekuwa yakifanyika katika pembe zote za dunia, ikiwemo huko Ujerumani ambapo mashindano hayo ya kandanda yanatazamiwa kufanyika katika msimu wa joto kali.

Kadhalika haya yanaarifiwa siku chache baada ya Kitengo cha Huduma ya Utekelezaji wa Nje ya Ulaya (EEAS) kusema kuwa, Umoja wa Ulaya umelazimika kubeba zigo zito la madeni kutokana na kuifuata kibubusa Marekani katika kuiunga mkono Ukraine kwenye vita na Russia.

Israel inatazamiwa kuchuana na Iceland huku Ukraine ikiratibiwa kuvaana na Bosnia Herzegovina mnamo Machi 21, katika mechi za kuwania kufuzu fainali hizo zijazo za michuano ya EURO 2024. Mashindano hayo ya kieneo yataanza mnamo Juni mwaka huu nchini Ujerumani.

Tags