Dunia yapongeza uamuzi wa ICJ dhidi ya Israel
Viongozi na taasisi mbalimbali za kimataifa duniani zimeendelea kupongeza uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) wa kuitaka Israel ichukue hatua zote zinazohitajika kuzuia vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.
Waziri Mkuu wa Palestina, Mohammad Shtayyeh ameashiria uamuzi huo uliotolewa jana Ijumaa na ICJ na kusema kuwa, "Hukumu ya mahakama hiyo ya Umoja wa Mataifa inathibitisha mwisho wa enzi za Israel kutowajibishwa kwa kukanyaja sheria."
Amesema ingawaje Wapalestina walitaraji kuwa ICJ ingeliagiza Israel isimamishe vita mara moja, lakini uamuzi wa mahakama hiyo ya mjini The Hague nchini Uholanzi hata hivyo umetuma ujumbe mzito kwa madola yanayouunga mkono utawala huo haramu.
Wakati huo huo, Volker Turk, Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kuhusiana na hukumu hiyo ya ICJ kwamba, "Israel inapaswa kutekeleza kikamilifu maamuzi ya ICJ kwa kuzingatia Hati ya Mauaji ya Kimbari. Tunazitaka pande zote husika kuheshimu na kutekeleza majukumu yake chini ya sheria ya kimataifa."
Kadhalika Rais wa Colombia, Gustavo Petro ameutaja uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki kuwa ushindi mkubwa kwa ubinadamu. "Ushindi kwa ubinadamu, Israel lazima izuie mauaji ya kimbari," ameandika Petro kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Mataifa mbali mbali duniani kama Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Qatar, Misri, Saudi Arabia na Jordan yamepongeza uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwa shauri la mashtaka ya Afrika Kusini dhidi ya Israel, unaoiamuru Israel iache vitendo vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina na kuchukua hatua za kuwasaidia raia.