Waingereza wataka Blair apelekewe ICC kwa kuivamia Iraq
Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu, asasi za kiraia na familia za wanajeshi wa Uingereza waliouawa nchini Iraq wamefanya maandamano katika mji mkuu London kulaani hatua ya Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo Tony Blair ya kuidhinisha uvamizi dhidi ya Iraq mwaka 2003 bila ya kuwepo sababu ya msingi.
Waandamanaji hao waliokuwa wamebeba mabango yenye picha za wahanga wa uvamizi huo wameitaka Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imfungulie mashtaka Blair kutokana na kile walichokitaja kuwa 'ugaidi na jinai za kivita'. Sarah O’Connor, dada ya Bob O’Connor, mwanajeshi wa Uingereza aliyeuawa nchini Iraq mwaka 2005 amesema "Magaidi walimuua kakangu, lakini hapo katika neno ugaidi najumuisha jina la Blair".
Maandamano hayo yamejiri baada ya jopo lililokuwa likichunguza nafasi ya Uingereza katika uvamizi dhidi ya Iraq kutoa ripoti iliyosema kuwa, serikali ya London haikutathmini kwa kina machaguo mengine ya amani yaliyokuwa mezani kabla ya nchi hiyo na Marekani kuivamia kijeshi Iraq mwaka 2003. Ripoti ya jopo hilo inayojulikana kama Uchunguzi wa Chilcot imesema Uingereza iliifuata kibubusa Marekani kuishambulia Iraq kwa kuzingatia taarifa zisizo na mashiko za kiintelijensia. Hii ni katika hali ambayo, licha ya Blair kukiri kuwa alifanya makosa na kusema kuwa yuko tayari kubeba dhima ya uamuzi wake huo wa kukurupuka sambamba na kuomba radhi familia za wahanga wa uvamizi huo, lakini anashikilia kuwa "dunia ni pahala salama bila uwepo wa Saddam Hussein".
Itakumbukwa kuwa, Marekani na Uingereza ziliivamia Iraq mwaka 2003 kwa kisingizio kuwa utawala uliopinduliwa wa dikteta Saddam Hussein ulikuwa unamiliki silaha za maangamizi (WMDs). Kati ya askari 120,000 wa Uingereza waliotumwa Iraq, 179 miongoni mwao waliuawa mbali na Wairaqi karibu milioni moja kuuawa na vilevile kuharibiwa miundomsingi ya nchi hiyo ya Kiarabu.