Jan 29, 2024 06:27 UTC
  • Ulimwengu wa Michezo, Jan 29

Huu ni mkusanyiko wa baadhi ya matukio makubwa yaliyoshuhudiwa viwanjani katika pembe mbali mbali za dunia ndani ya siku saba zilizopita.....

Kombe la Asia; Iran yatinga hatua ya muondoano

Timu ya taifa ya soka ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetinga hatua ya muondoano katika michuano ya fainali za Kombe la Asia nchini Qatar. Jamhuri ya Kiilamu imetinga kibabe hatua hiyo ya mchujo baada ya kuichabanga Imarati mabao 2-1 katika mchuano wa raundi ya 16. Mshambuliaji nyota wa kimataifa anayekipiga huko Porto, Mehdi Taremi ndiye aliyeifungia Iran mabao hayo katika dakika ya 26 na 65 ya mchezo. Vijana hao wa Kiirani walifunga mabao mengine matatu, lakini yalikataliwa baada ya refa kupata ushauri wa refa msaidizi wa kielektroniki VAR. Kabla ya hapo, Team Melli kama inavyofahamika hapa nchini, iliizaba Hong Kong bao moja bila jibu katika mchuano wake wa pili wa Kndi C uliopigwa katika Uwanja wa Kimataifa wa Khalifa huko al-Rayyan nchini Qatar. Aidha Iran ilifanikiwa kuichabanga Palestina mabao 4-1 katika mchezo wa ufunguzi uliopigwa katika Uwanja wa Jiji la Elimu huko huko al-Rayyan nchini Qatar. Iran inasalia kileleni mwa Kundi C ikiwa na alama 9. 

 

Vijana hao wa Kiirani wanaonolewa na Amir Ghalenoei wamepangwa katika Kundi C pamoja na Imarati, Palestina na Hong Kong kwenye michuano hiyo ya kibara inayoendelea huko Qatar. Team Melli ya Iran ambayo inapania kuhitimisha ukame wa miaka 47 wa kutwaa taji hilo la kieneo, inatazamiwa kushuka dimbani kuvaana na Syria Jumatano ya Januari 31. Kwengineko, Australia siku ya Jumapili iliizaba Indonesia mabao 4-0 na kutinga hatua ya robofainali ya mashindano hayo ya kibara.  Australia sasa itakutana na mshindi wa mechi ya Jumanne baina ya Saudi Arabia na Korea Kusini. Tajikistan pia imesogea mbele kwa kuicharaza Imarati mabao 5-3 katika upigaji matuta, baada ya dakika ada za nyongeza kumalizika kwa bao 1-1.

AFCON; Mkondo wa 16-bora, makocha watimuliwa

Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) ilichukua mapumziko ya siku mbili na kuendelea kuroroma tena Jumamosi ya Januari 27, ambapo pazia lake lilifunguliwa kwa mchuano kati ya Super Eagles ya Nigeria na Indomitable Lions ya Cameroon. Nigeria wametinga hatua ya Robo Fainali ya michuano hiyo ya kikanda baada ya kuigaragaza Cameroon mabao 2-0 katika mchuano huo wa hatua ya 16 Bora. Mabao yote 2 ya Super Eagles yalifungwa na Ademola Lookman katika dakika ya 39 na 90 ya mchezo.

Huku mkondo wa 16 bora wa Afcon ukiendelea, wakufunzi sita wa timu za Afrika zilizoshiriki Afcon huko Kodivaa tayari wamepoteza kazi. Makocha kutakiwa kufanya vyema katika michuano hii ni ishara kuwa hali ya mchezo wa mpira wa miguu Afrika ipo katika hatua za kustawi. Makocha wa Ghana, Ivory Coast, Algeria, Tanzania, Gambia na Tunisia ama wamepigwa kalamu nyekundu au kulazimika kujiuzulu kwa sababu ya matokeo yasiyo ya kuridhisha kwenye mashindano hayo makubwa ya soka barani Afrika. Angola imesogea mbele kibabe baada ya kuinyoa kwa chupa Zambia kwa kuigaragaza mabao 3-0 katika mchuano mwingine wa mkondo wa 16-bora. Mwakilishi wa Afrika Mashariki kwenye mashindano hayo, timu ya kandanda ya Tanzania, Taifa Stars, iliaga michuano hiyo baada ya kutoka sare tasa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

 

Huku Tanzania ikirejea Dar es Salaam, DRC imefanikiwa kumalizika ya pili katika Kundi F, baada ya kuibandua miamba ya soka barani Misri nje ya michuano hiyo Jumapili ya Januari 28. Timu hizo zilitoa sare ya bao 1-1 katika dakika za ada na nyongeza, yaliyofungwa na Meshack Elia katika dakika ya 37 kabla ya Mostafa Muhammad kuwasawazishia Mafarao kupitia mkwaju wa penati katika dakika za majeraha, kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza. Upigaji matuta ulimalizika kwa batoto ba Kongo kucheka na nyavu mara 8 huku Waarabu wa Misri wakizitikisa mara 7.  Ijumaa ijayo mjini Abidjan, DRC itavaana na Guinea ambayo Jumapili iliwatandika majirani zao Guinea ya Istiwa bao 1-0, kusaka tiketi ya nusu fainali. Morocco watakabana koo na Afrika Kusini Jumanne hii ya Janauri 30, katika mkondo huo wa kufa kupona.

Riadha; Kenya yatamalaki mbio za Marrakech, Sevilla

Mwanariadha nyota wa Kenya, Sammy Kitwara ameibuka mfalme wa mbio za Marrakech Marathon na kujizolea dola 10,000 Sh milioni 1.6 za Kenya kwenye mbio hizo zilizovutia washiriki 12,000 nchini Morocco, Jumapili ya Januari 28. Kitwara alikamilisha mbio hizo za kilomita 42 kwa kutumia saa 2, dakika 7 na sekunde 53 akifuatiwa kwa karibu na Wamorocco Omar Ait Chitachen na Mustapha Houdadi. Wakati huo huo, Wakenya Bravin Kiprop na Vincent Kipkorir wamefagia nafasi mbili za kwanza katika mbio za kilomita 21 za Sevilla kwa kutumia dakika 59 na sekunde 21 na dakika 59 na sekunde 48 kwa usanjari huo nchini Uhispania. Mwitaliano Iliass Aouani alifunga tatu-bora kwa saa 1:01:32.

 Dondoo za Hapa na Pale

Rais wa Muungano wa Mashirikisho ya Soka ya Ulaya (UEFA) amesema kushiriki Israel na Ukraine katika fainali zijazo za michuano ya EURO 2024 ni hatari kwa usalama. Aleksander Ceferin, Rais wa UEFA ameiambia Telegraph Sports kuwa, kushiriki Israel na Ukraine kwenye mechi za EURO 2024 kunaweza kuwa tishio la usalama kwa mashindano hayo ya kieneo yanayotazamiwa kufanyika katika msimu wa joto kali nchini Ujerumani. Caferin ameeleza bayana kuwa, "Katika nyakati hizi za kiwendawazimu, ambapo kijiopolitiki dunia imewehuka, wasi wasi mkubwa uliopo ni masuala ya usalama." Ameendelea kusema: Hofu yangu si tu viwanjani, kwa kuwa naamini viwanja vitapewa ulinzi wa kutosha, lakini mashabiki wa kila aina watazagaa kote kwenye majiji na miji (ya Ujerumani). Rais wa UEFA ametoa indhari hiyo katika hali ambayo, chuki dhidi ya Wazayuni zimeongezeka kote duniani kufuatia vita vya utawala haramu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Aleksander Ceferin, Rais wa UEFA 

 

Maandamano ya kulaani jinai hizo za Israel huko Gaza yamekuwa yakifanyika katika pembe zote za dunia, ikiwemo huko Ujerumani ambapo mashindano hayo ya kandanda yanatazamiwa kufanyika katika msimu wa joto kali. Israel inatazamiwa kuchuana na Iceland huku Ukraine ikiratibiwa kuvaana na Bosnia Herzegovina mnamo Machi 21, katika mechi za kuwania kufuzu fainali hizo zijazo za michuano ya EURO 2024. Mashindano hayo ya kieneo yataanza mnamo Juni mwaka huu nchini Ujerumani.

Kwengineko, bondia nyota wa Tanzania Hassan Mwakinyo amefanikiwa kutwaa taji la mkanda wa WBO na kuipaisha nchi hiyo ya Afrika Mashariki katika ulimwengu wa masumbwi. Mwakinyo akiwa katika Uwanja wa Amaan Complex Visiwani Zanzibar Jumamosi, alifanikiwa kushinda kwa KO katika raundi ya 7, kwa kumdondosha mpinzani wake Mbiya Kanku wa Ghana. Baada ya ushindi huo, Mwakinyo alipokewa kifalme jijini Dar es Salaam na mashabiki pamoja na wananchi

Mbali na hayo, meneja wa zamani wa Real Madrid, Zinedine Zidane almaarufu ‘Zizou’ amepiga chini ofa ya kuwa kocha mkuu wa Timu ya Taifa ya Algeria. Hii inakuja baada ya Chama cha Soka Algeria (FA) kumwekea ofa nono ambayo ingemfanya kuwa kocha anayelipwa kitita kikubwa zaidi Afrika. Zidane ambaye ni mzaliwa wa Ufaransa kwenye asili ya Algeria alitakiwa kwa ajili ya kuchukua mikoba ya Djamel Belmadi aliyejiuzulu baada ya Algeria kusukumizwa nje ya AFCON 2023 kwenye hatua ya makundi.

Zinedine Zidane

 

Na Kocha wa Liverpool, Jürgen Klopp ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo mwishoni mwa msimu huu. Baada ya kuiongoza ‘The Reds’ kwenye fainali nyingine ya Carabao Cup dimba la Wembley Jumatano usiku, Klopp ,56, ataendelea kusimamia mechi zilizosalia za timu hiyo msimu huu. Wasimamizi wasaidizi Pepijn Lijnders na Peter Krawietz, pamoja na mkufunzi wa maendeleo, Vitor Matos, pia wataacha nyadhifa zao mwishoni mwa msimu huu, huku Lijnders akitaka kuendeleza taaluma yake ya usimamizi. Klopp aliteuliwa kuwa meneja wa Liverpool mnamo Oktoba 8, 2015. Ulikuwa uamuzi ambao ungebadilisha klabu na kuifanya kuwa tishio ndani na nje ya Uingereza. Chini ya usimamizi wake, Liverpool wametwaa Ligi ya Klabu Bingwa (UEFA Champions League), Ligi Kuu ya Uingereza EPL, FIFA Club World Cup, FA Cup, League Cup na UEFA Super Cup, pamoja na FA Community Shield (Ngao ya Jamii).

………………….MWISHO……………

 

 

Tags