Jan 31, 2024 10:51 UTC
  • Volodomir Zelensky
    Volodomir Zelensky

Rais wa Ukraine amekiri kuwa jeshi la nchi hiyo ni dhaifu mkabala wa Russia na kusema: Ulaya peke yake haiwezi kuisaidia Ukraine dhidi ya Russia bila uungaji mkono wa Marekani.

Akihojiwa na televisheni ya Ujerumani, Rais Volodomir Zelensky wa Ukraine ameeleza bayana kuwa iwapo Marekani itapunguza misaada yake kwa Ukraine kuna uwezekano Ulaya ikashindwa kuisaidia Kyiv iwe ni kifedha na au kijeshi.  

Rais wa Ukraine ameeleza kuwa, tangu kuanza mwaka huu wa 2024 Russia imevurumisha kuelekea upande wa Ukraine zaidi ya makombora 330 na karibu ndege zisizo na rubani (droni) 600. Amesisitiza kuwa kudhibiti na kulinda anga ya Ukraine ni muhimu sana, lakini hili halitawezekana bila msaada wa washirika wetu, hasa misaada ya silaha kutoka Marekani. 

Awali Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba, alidokeza kwamba raia wengi nchini Ukraine wana wasiwasi kuwa msaada wa kifedha wa Washington kwa Kyiv utakatizwa iwapo Trump atashinda tena uchaguzi wa Rais wa Marekani. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Ukraine, Dmytro Kuleba

Kyiv inajiandaa kwa matokeo ya uchaguzi wa Marekani, ili iwapo mgombea wa chama cha Republican atashinda iendelee kunufaika na misaada ya Marekani na NATO. Viongozi wa Ukraine wanafahamu vyema kwamba, katika hali ngumu ya vita wanalazimika kutoa jibu chanya kwa kila ombi la Magharibi ili waweze kupatiwa misaada na nchi hizo hata kama matakwa hayo yatakuwa kinyume na maslahi ya wananchi na mustakabali wa Ukraine. 

Tags